WACHIMBAJI WADOGO VIJANA 4000 KUPEWA LESENI ZA UCHIMBAJI MADINI WILAYANI BUKOMBE - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Tuesday, December 23, 2025

WACHIMBAJI WADOGO VIJANA 4000 KUPEWA LESENI ZA UCHIMBAJI MADINI WILAYANI BUKOMBE



Na Mwandishi Wetu, Bukombe, Geita


Serikali kupitia Wizara ya Madini chini ya utekelezaji wa Programu ya Mining for A Brighter Tommorow (MBT) imeweka utaratibu mzuri na kugawa leseni kwa vikundi vya wachimbaji wadogo wanawake na vijana takribani 4000 kwa ajili ya shughuli za uchimbaji.

Hayo yameelezwa leo Desemba 23, 2025 na Waziri wa Madini, Mheshimiwa Anthony Mavunde wakati akizungumza katika mkutano wa hadhara na wachimbaji katika machimbo ya Msasa, Wilayani Bukombe.

"Mh. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ametuelekeza kuhakikisha tunawasimamia na kuwapanga wachimbaji wadogo ikiwa ni pamoja na kuwapatia maeneo ya uchimbaji ili kurasimisha shughuli zao.

"Na ndiyo maana sisi kama Wizara ya Madini, tunaendelea na uchambuzi ili kubaini leseni zote zisizoendelezwa tuweze kuzifuta kwa mujibu wa Sheria ya Madini Sura 123 na kugawa maeneo hayo kwa wachimbaji wenye nia ya dhati kuyaendeleza.

Waziri Mavunde aliongeza kuwa, Serikali inatambua mchango wa wachimbaji wadogo wa madini kwenye Pato la Taifa ambao zaidi ya asilimia 40 ya mapato ya sekta ya madini yanatokana na shughuli za uchimbaji mdogo, hivyo inaendelea kutatua changamoto mbalimbali za wachimbaji wadogo hususan katika masuala tozo na ushuru mbalimbali zilizopo katika migodi midogo.

Pia, Mhe. Mavunde ameeleza kuwa , kwa kutambua mchango wao, Serikali kupitia Tume ya Madini itakabidhi leseni ya utafiti iliyokuwa iliyokwisha muda wake karibu na eneo hili la Msasa ili kuwapanga na kuwawezesha wachimbaji wadogo kumiliki leseni kwa vikundi na kuendeleza uchimbaji bila kunyanyasika.

Akisisitiza juu ya usawa kwa wachimbaji wanaohitaji leseni, Mhe. Mavunde alieleza kuwa kila Mtanzania anayo haki Sawa ya kumiliki leseni ya uchimbaji madini, na ndiyo maana Serikali imekuja na utaratibu wa kimfumo ambao unawezesha mtu yeyote kuomba leseni ya madini na kupatiwa pasipo upendeleo wowote.

Naye, Mkuu wa Mkoa wa Geita , Mh. Martine Shigela amesema kuwa, kwa upande wa Serikali ya Mkoa wa Geita inatambua changamoto ya umeme katika machimbo ya Msasa, na tayari wapo mbioni kukamilisha utatuzi huo kwa kuleta umeme katika machimbo hayo ili kuchagiza uzalishaji na kupunguza gharama za uendeshaji kwa wachimbaji.

Mhe. Shigela alimwahidi Mhe. Mavunde kuwa ataendelea kuwa karibu na wachimbaji wa Mkoani Geita ili kuhakikisha wananufaika na shughuli zao, Serikali inapata mapato na anatatua changamaoto zao kwa wakati.

Kwa upande wake, Rais wa Shirikisho la Wachimbaji Wadogo wa Madini Tanzania (FEMATA), Bw. John Bina
aliishukuru Serikali kwa kuendelea kuwa bega kwa bega na wachimbaji wadogo na kusisitiza kuendelea kutoa ushirikiano kwa mamlaka zote zinazosimamia uchimbaji ili wachimbaji wadogo wafanye shughuli za uzalishaji bila changamoto yeyote.


No comments:

Post a Comment