
Na Shua Ndereka, OKULY BLOG, Morogoro
Jumla ya mashauri 770 kati ya mashauri 1,116 yaliyokuwepo katika Mahakama Kuu Kanda ya Morogoro yamefanikiwa kumalizika, huku mashauri 346 yakibaki sawa na asilimia 69, ambapo kati ya mashauri hayo, mashauri 13 pekee ndiyo yaliyozidi miezi 12 tangu yalipofunguliwa.
Mashauri hayo yalijumuisha mashauri 298 yaliyosalia kutoka Desemba 2024 pamoja na mashauri 818 yaliyofunguliwa mwaka 2025.
Akizungumza katika maadhimisho ya Siku ya Sheria nchini, yaliyofanyika hivi karibuni mkoani Morogoro, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Morogoro, Mhe. Rose Ebrahim, amesema mafanikio hayo yanatia moyo na kuonesha ufanisi wa Mahakama katika utoaji wa haki kwa wakati.
Amesema, ufanisi huo unatokana na ushirikiano mzuri kati ya wadau wa haki pamoja na juhudi na dhamira ya Majaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Morogoro, jambo linalochangia kuimarisha mazingira rafiki ya uwekezaji kwa Mkoa wa Morogoro na Taifa kwa ujumla.
Jaji Rose ameeleza kuwa, mashauri yaliyomalizika mwaka 2025 yalihusisha masuala muhimu yanayogusa uchumi wa Taifa, maslahi ya wawekezaji pamoja na ustawi wa wananchi.
“Wadau wa mnyororo wa haki madai wanakumbuka kuwa, kuanzia Novemba hadi Desemba 2025, tulifanya vikao maalumu vya kusikiliza mashauri ya aina hii. Katika kipindi hicho, jumla ya mashauri 47 yalisikilizwa na kuamuliwa, yenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 7. Bila mikakati hii, fedha hizo zisingeweza kuwa katika mzunguko wa uzalishaji kwa sasa,” amesema.
Katika ngazi ya Mahakama ya Hakimu Mkazi, amesema kwa mwaka 2024 zilibakia mashauri 49, huku mashauri 95 yakifunguliwa mwaka 2025, Mashauri 125 yalisikilizwa na kufanya jumla ya mashauri yaliyobaki kuwa 19, sawa na asilimia 87 ya umalizwaji wa mashauri yote. Kati ya mashauri hayo, shauri moja pekee ndilo lililozidi miezi sita tangu lilipofunguliwa.
Aidha, kwa Mahakama za Wilaya, mashauri 296 yalibaki mwaka 2024, mashauri 1,697 yalifunguliwa mwaka 2025, huku mashauri 1,852 yakisikilizwa, na kusababisha mashauri yaliyobaki kuwa 141 sawa na asilimia 93 ya umalizwaji wa mashauri yote. Kati ya mashauri hayo, mashauri 9 pekee ndiyo yaliyozidi miezi sita.
Kuhusu mwelekeo wa utekelezaji wa majukumu kwa mwaka 2026, Jaji Rose Ebrahim amesema Mahakama Kuu Kanda ya Morogoro itaendelea kuimarisha utoaji wa huduma bora, kuongeza weledi, bidii na ufanisi katika kazi pamoja na kuimarisha matumizi ya TEHAMA katika ngazi zote za mahakama.
Amesema pia juhudi zitaendelea kufanyika katika ukarabati na uboreshaji wa miundombinu ya mahakama, hususan mahakama za mwanzo, ili kuweka mazingira rafiki kwa watumishi na watumiaji wa huduma za mahakama.

Katika hatua nyingine Mgeni maalum katika sherehe hizo ambaye ni Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Adam Kighoma Malima, ameishauri Mahakama Kuu Kanda ya Morogoro kurejesha utaratibu wa kuadhimisha Wiki ya Sheria badala ya kuishia kwenye Siku ya Sheria pekee.
Malima amesema kuwa, utaratibu wa Wiki ya Sheria uliwahi kuleta mafanikio makubwa kutokana na wananchi kupata elimu ya kisheria kwa karibu kupitia mabanda ya elimu mitaani, matumizi ya vyombo vya habari na kuwafuata wananchi moja kwa moja katika maeneo yao.
“Ningeomba mfumo wa sheria wa Morogoro urudishe wiki ya Sheria badala ya Siku ya Sheria pekee, kwani ulikuwa na mafanikio makubwa kwa kuwafikia wananchi na kuwapatia elimu kuhusu mifumo ya Mahakama”Amesema Malima.

Naye Mwenyekiti wa Chama cha Mawakili Tanganyika (TLS) Mkoa wa Morogoro, Wakili Baraka Lweeka, amesema TLS itaendelea kutoa msaada wa kisheria kwa wananchi wenye uhitaji ili kuhakikisha haki inapatikana bila vikwazo.
Amesema kwa mwaka 2025, TLS ilihudumia watu 421, ambapo 209 walipata ushauri wa kisheria, 102 walipewa mawakili wa uwakilishi mahakamani na 110 walipewa elimu ya kisheria.
Wakili Lweeka amesisitiza umuhimu wa kuwalinda mawakili wa kujitegemea na kuimarisha uhuru wa mahakama, akisema hayo ndiyo msingi wa utawala wa sheria, haki, amani na uwajibikaji.
Aidha, amepongeza maboresho makubwa yaliyofanywa na Mahakama ya Tanzania katika matumizi ya mifumo ya TEHAMA na uwazi katika utoaji wa haki.
Kwa upande wake, Jaji Mfawidhi Rose Ebrahim amelipokea ombi la kurejeshwa kwa Wiki ya Sheria na kuahidi kuwa Mahakama Kuu Kanda ya Morogoro itakuja na mikakati mipya ya kuadhimisha Wiki ya Sheria kwa lengo la kuwafikia wananchi kwa karibu zaidi.
Maadhimisho hayo yalifanyika katika viwanja vya Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki (IJC) Kanda ya Morogoro, yakihusisha viongozi wa Serikali, Mahakama, taasisi za sheria, viongozi wa dini pamoja na wananchi, yakiwa na kauli mbiu ya mwaka 2026 isemayo “Mchango wa Mahakama katika Ustawi wa Maendeleo ya Taifa.”






No comments:
Post a Comment