𝐖𝐀𝐁𝐔𝐍𝐆𝐄 𝐖𝐀𝐂𝐇𝐀𝐑𝐔𝐊𝐀 𝐁𝐔𝐍𝐆𝐄𝐍𝐈, 𝐖𝐀𝐓𝐀𝐊𝐀 𝐍𝐄𝐌𝐂 𝐊𝐔𝐏𝐄𝐖𝐀 𝐌𝐄𝐍𝐎 - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Wednesday, April 22, 2026

𝐖𝐀𝐁𝐔𝐍𝐆𝐄 𝐖𝐀𝐂𝐇𝐀𝐑𝐔𝐊𝐀 𝐁𝐔𝐍𝐆𝐄𝐍𝐈, 𝐖𝐀𝐓𝐀𝐊𝐀 𝐍𝐄𝐌𝐂 𝐊𝐔𝐏𝐄𝐖𝐀 𝐌𝐄𝐍𝐎

Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wameibuka na hoja nzito wakichangia bajeti ya Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), wakitaka Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) kupewa mamlaka kamili pamoja na rasilimali za kutosha ili liweze kutekeleza majukumu yake ipasavyo.

Wakichangia kwa nyakati tofauti baada ya hotuba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Mhandisi Hamad Y. Masauni, wabunge hao walisema licha ya NEMC kupewa jukumu la kusimamia na kulinda mazingira chini ya Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), bado haina nguvu ya kisheria ya kutosha kuchukua hatua kali dhidi ya waharibifu wa mazingira.

Akichangia mada hiyo, Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Tabora, Mhe. Christina Mndeme, alimpongeza Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuiwezesha NEMC kupata maabara inayotembea, akisema hatua hiyo itaongeza ufanisi katika udhibiti wa mazingira kwa kutumia ushahidi wa kisayansi.

Aidha, alisisitiza kuwa endapo NEMC itapewa mamlaka kamili, uwajibikaji utaongezeka, ufanisi utaimarika na taasisi hiyo itakuwa na uwezo wa kutekeleza majukumu yake kisheria bila muingiliano wowote kutoka taasisi nyingine.

Naye Mbunge wa Katavi, Mhe. Thomas Kampala, alipoongea alisisitiza kuwa ipo haja ya haraka ya kuipa NEMC “meno” ili iweze kuchukua hatua stahiki dhidi ya vitendo vya uharibifu wa mazingira vinavyoongezeka nchini. Alieleza kuwa kwa sasa taasisi hiyo inakosa nguvu ya kisheria hata inapobaini ukiukwaji mkubwa wa Sheria za mazingira.

Kadhalika Mbunge wa Bumbuli, Mhandisi Ramadhan Hamza Singano, aliongeza kuwa pamoja na NEMC kufanya kaguzi katika sekta mbalimbali ikiwemo migodi, gesi na mafuta, bado inakabiliwa na uhaba wa rasilimali kutokana na mgao mdogo wa bajeti.

Kwa upande wake, Mbunge wa Arumeru Mashariki, Mhe. Joshua Nassari, aliunga mkono hoja hiyo akitaka Serikali kuchukua hatua za makusudi kuimarisha NEMC ili iweze kusimamia kikamilifu uhifadhi wa mazingira.

Wabunge hao walisisitiza kuwa bila kuipa NEMC mamlaka kamili na rasilimali za kutosha, jitihada za kulinda mazingira nchini zitabaki kuwa dhaifu.

No comments:

Post a Comment