BoT YAWANOA WALEMAVU SINGIDA KUHUSU ELIMU YA FEDHA - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Friday, April 24, 2026

BoT YAWANOA WALEMAVU SINGIDA KUHUSU ELIMU YA FEDHA


Katika mkakati wa kuwa na uchumi jumuishi unaochangiwa na makundi yote ndani ya jamii, Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imetoa mafunzo ya elimu ya fedha kwa kundi maalumu la walemavu mkoani Singida.

Elimu hiyo iliyohusisha majukumu ya BoT, elimu ya fedha, utambuzi wa alama za usalama wa noti na sarafu pamoja na mbinu sahihi za utunzaji wa fedha ilitolewa Alhamisi Aprili 23, 2026.

Akizungumza katika mafunzo hayo, Mkurugenzi Mtendaji wa taasisi ya walemavu ya PPD (Patronage for People with Disability), Bw. Ramadhan Maulid, alisema elimu inayotolewa na BoT ina mchango mkubwa kwa makundi maalumu, hususan watu wenye ulemavu, kwa kuwawezesha kuelewa fursa za kiuchumi na majukumu ya benki hiyo.

“Tunapongeza Benki Kuu kwa kuimarisha uchumi wa nchi kupitia utoaji wa elimu za fedha kwa makundi maalumu, hususan sisi watu wenye ulemavu. Elimu hizi zinatusaidia kutambua fursa za kiuchumi na kutufanya tushiriki kikamilifu katika uchumi wa nchi bila kuachwa nyuma,” alisema Bw. Maulid.

Mada za mafunzo hayo yaliyowashirikisha zaidi ya washiriki 100, ziliwasilishwa na Meneja Msaidizi wa Sarafu kutoka BoT Tawi la Dodoma, Bi. Matilda Luvinga, pamoja na Afisa Mwandamizi, Bw. Sadi Makomba.

Hatua hiyo ni sehemu ya jitihada endelevu za BoT katika kuhakikisha wananchi wa makundi yote wanapata elimu ya kifedha, ili kuwawezesha kushiriki kikamilifu katika shughuli za kiuchumi na kuchangia utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo ya Mwaka 2050.

No comments:

Post a Comment