Na: OWM TAMISEMI, Dodoma
Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu TAMISEMI, Dkt. Jafar Seif, amewataka Maafisa Lishe nchini kuongeza jitihada katika kukabiliana na changamoto za lishe na magonjwa yanayotokana na lishe duni, akieleza kuwa hali ya lishe bado si ya kuridhisha. Dkt. Seif alibainisha kuwa kati ya watoto 10 wenye umri chini ya miaka mitano, watatu wanakabiliwa na udumavu na asilimia 58 wanakabiliwa na upungufu wa damu.
Akihutubia Mkutano wa Mwaka wa Uratibu wa Huduma za Lishe uliowaleta pamoja Maafisa Lishe kutoka Halmashauri zote 184 na Mikoa 26 ya Tanzania Bara Jijini Dodoma hivi karibuni, Dkt. Seif alisema hatua za haraka zinahitajika kubadili mwenendo wa viashiria vya lishe. Aliwataka wataalam hao kuongeza uwajibikaji katika utekelezaji wa afua za lishe ili kufikia mabadiliko yanayohitajika.
Dkt. Seif pia alieleza kuwa tatizo la upungufu wa damu limeathiri asilimia 56 ya wanawake wajawazito na asilimia 42 ya wanawake wenye umri wa kuzaa (kati ya miaka 15-49).
Aidha, alisema asilimia 36 ya wanawake wa miaka 20-49 wana uzito uliopindukia, wakati wanaume wa kundi hilo la umri asilimia 17 wanakabiliwa na tatizo la uzito uliopindukia, hali inayochangia kuongezeka kwa magonjwa sugu yasiyoambukizwa kama kisukari, shinikizo la damu na magonjwa ya moyo.
Kuhakikisha Maafisa Lishe wanaweza kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi, Dkt. Seif alisema Serikali itaendelea kuchukua hatua mbalimbali ikiwemo kuongezwa kwa uwekezaji katika sekta ya lishe. Bajeti ya lishe imeripotiwa kuongezeka kutoka Shilingi Bilioni 2 mwaka wa fedha 2017/2018 hadi kufikia Bilioni 20.3 kwa mwaka wa fedha 2025/2026.
Aidha, Dkt. Seif alisema serikali imeongeza nguvu kazi kwa kuajiri maafisa lishe 654 ambao wamepangiwa vituo vya kazi katika mikoa na mamlaka za serikali za mitaa kote nchini.
Alisisitiza umuhimu wa ubora wa takwimu, kuimarisha mpango wa chakula shuleni na kusimamia utekelezaji wa kanuni za uongezaji wa virutubisho kwenye vyakula ili kupunguza athari za matatizo ya lishe nchini.
Maafisa Lishe pia waliagizwa kusimamia matumizi ya rasilimali zilizotengwa kwa ajili ya lishe, pamoja na kuimarisha utoaji wa elimu kwa jamii ili kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu lishe bora na madhara ya utapiamlo. Dkt. Seif aliwataka wataalam hao kuhakikisha afua za lishe zinafanyika kwa ufanisi na kwa uwazi ili kuleta mabadiliko ya kudumu katika afya ya wananchi.
Wataalam wa lishe na wadau wanatarajiwa kuendelea kufanya kazi kwa ushirikiano na serikali za mitaa ili kutekeleza mipango makini ya kupunguza udumavu, upungufu wa damu na kuzuia kuongezeka kwa magonjwa sugu yasiyoambukizwa kupitia sera, utoaji wa huduma na elimu endelevu kwa jamii.




No comments:
Post a Comment