DKT. CHAYA ASISITIZA USHIRIKI WA WANANCHI KUTEKELEZA DIRA 2050 - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Saturday, April 11, 2026

DKT. CHAYA ASISITIZA USHIRIKI WA WANANCHI KUTEKELEZA DIRA 2050


Naibu Waziri wa Ofisi ya Rais – Mipango na Uwekezaji, Dkt. Pius Chaya,akitoa mada katika mhadhara ulioandaliwa na Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini (IRDP), Aprili 10,2026 jijini Dodoma


Na Okuly Julius, OKULY BLOG, DODOMA



Naibu Waziri wa Ofisi ya Rais – Mipango na Uwekezaji, Dkt. Pius Chaya, amesisitiza umuhimu wa ushiriki wa kila Mtanzania katika utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 ili kufikia malengo makubwa ya kiuchumi, ikiwemo kujenga uchumi wa dola za Marekani trilioni moja.

Akitoa mada katika mhadhara ulioandaliwa na Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini (IRDP), Aprili 10,2026 jijini Dodoma, Dkt. Chaya amesema mafanikio ya dira hiyo yanategemea utekelezaji wa vitendo kuanzia ngazi ya kijiji hadi taifa.

Amebainisha kuwa Serikali, kupitia Tume ya Taifa ya Mipango, imejipanga kuhakikisha kunakuwa na ufuatiliaji na tathmini ya kila hatua ya utekelezaji.

Aidha, amewahimiza wanataaluma kufanya tafiti zenye tija zinazolenga kutatua changamoto za wananchi badala ya kubaki kwenye makabrasha, akieleza kuwa maarifa hayo ni nyenzo muhimu katika kufanikisha Dira ya Maendeleo 2050.

Dkt. Chaya amesema Serikali imeandaa mfumo unaoimarisha uhusiano kati ya viwanda, wazalishaji na vyuo vya elimu ya juu nchini, ili kuhakikisha wahitimu wanaozalishwa wanakidhi mahitaji halisi ya soko la ajira. Amesema hatua hiyo imewezekana kupitia mikataba mbalimbali kati ya Serikali na sekta ya uzalishaji, hususan viwanda.

“Ili chuo kizalishe wahitimu watakaoingia moja kwa moja kwenye soko la ajira, ni lazima soko lenyewe lieleze linahitaji wataalamu wa aina gani,” amesema Dkt. Chaya.

Kwa upande wake, Mkuu wa Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini, Prof. Hozen Mayaya, amesema taasisi hiyo itaendelea kuandaa wahitimu watakaosaidia kikamilifu utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

Amesema wanawajengea uwezo wa kujitegemea na kushirikiana na Serikali katika kuboresha mipango ya uwekezaji.

Aidha, Prof. Mayaya ameeleza kuwepo kwa changamoto kubwa katika upangaji wa ardhi nchini, akibainisha kuwa takribani asilimia 72 ya ardhi bado haijapimwa.

Amesema chuo hicho kinazalisha wataalamu wa mipango miji watakaosaidia kuziba pengo hilo na kuimarisha matumizi bora ya rasilimali ardhi.

Nao baadhi ya wanafunzi walioshiriki mhadhara huo, akiwemo Stumai Nyembo na Manyangu Gasuma, wamesema wako tayari kushiriki kikamilifu katika utekelezaji wa Dira ya Maendeleo 2050, wakieleza kuwa taaluma wanazopata zinalenga moja kwa moja kusaidia Serikali katika mipango ya uwekezaji na upangaji wa ardhi.




No comments:

Post a Comment