KAPINGA: SERIKALI KUENDELEA KUWAWEZESHA WANAWAKE KIUCHUMI - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Sunday, April 12, 2026

KAPINGA: SERIKALI KUENDELEA KUWAWEZESHA WANAWAKE KIUCHUMI

NA EMMANUEL MBATILO, DAR ES SALAAM

Waziri wa Viwanda na Biashara, Judith Kapinga, amesema Serikali itaendelea kuweka mazingira rafiki kwa wanawake wajasiriamali kwa kuwaondolea vikwazo na kurahisisha taratibu za urasimishaji wa biashara ili waweze kushiriki kikamilifu katika uchumi wa taifa.

Dkt. Kapinga ameyasema hayo leo Aprili 12, 2026 Jijini Dar es Salaam wakati akizungumza katika Maadhimisho ya Women In Balance Kitchen Party Gala 2026, akieleza kufurahishwa kwake kushiriki kwa mara ya kwanza katika jukwaa hilo linalowaunganisha wanawake wajasiriamali kutoka ngazi mbalimbali.

Amebainisha kuwa jukwaa hilo limekuwa na mchango mkubwa kwa zaidi ya miaka 16 kwa kuwaunganisha wanawake wenye mitaji midogo, ya kati na hata wanaojihusisha na biashara za ndani na nje ya nchi, hali inayochochea maendeleo yao kijamii na kiuchumi.

“Jukwaa hili ni muhimu sana kwa maendeleo ya wanawake kijamii na kiuchumi. Limekuwa mstari wa mbele katika kuwaunganisha na kuwawezesha wanawake kuinuana,” amesema Waziri Kapinga.

Akizungumzia changamoto zinazowakabili wanawake, Waziri Kapinga amesema bado wapo wanaohofia kurasimisha biashara zao kutokana na mtazamo wa ugumu wa taratibu. Hata hivyo, alisisitiza kuwa Serikali imebadili mwelekeo na sasa inalenga kuwawezesha wafanyabiashara badala ya kuwaadhibu.

“Zama za kufungia biashara zimekwisha. Tukimkuta mama anafanya biashara bila leseni, tutamwelekeza na kumsaidia kupata vibali vinavyohitajika. Lengo letu ni kuwawezesha, si kuwaadhibu,” amesisitiza.

Aidha, ameeleza kuwa Serikali inaendelea kuboresha utoaji wa huduma kwa kusogeza karibu taasisi zinazohusika na biashara, hatua inayolenga kurahisisha upatikanaji wa huduma kwa wafanyabiashara, hususan wanawake na vijana.

Katika hatua nyingine, Waziri Kapinga amewahimiza wanawake kuchangamkia fursa zilizopo katika sekta ya viwanda vidogo, vya kati na vikubwa, akisisitiza kuwa wao ni sehemu muhimu ya utekelezaji wa maono ya taifa ya kujenga uchumi imara.

Ameongeza kuwa sekta binafsi ina mchango mkubwa katika ukuaji wa uchumi, huku akiwahamasisha wanawake kuwa mstari wa mbele katika biashara na uwekezaji.

“Wanawake ni jeshi kubwa. Tukiamua, tunaweza. Mafanikio ya mwanamke yako mikononi mwake kupitia ushirikiano na kujituma,” amesema.

Aidha, amepongeza waandaaji wa jukwaa hilo kwa kuendelea kuwa chachu ya kuwawezesha wanawake kiuchumi na kijamii, na kuahidi kuwa Serikali itaendelea kushirikiana nao katika juhudi za kuinua wanawake.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Women In Balance Kitchen Party Gala 2026Vida Nasari, amesema washiriki 200 walihudhuria tukio hilo na wengi wao ni wanawake wenye ushawishi katika jamii.

Amesema washiriki hao wako tayari kushirikiana na taasisi zilizo chini ya Wizara ya Viwanda na Biashara, ikiwemo BRELASIDOTANTRADECBETBS na FCC, ili kupata elimu na taarifa sahihi zitakazowawezesha kusonga mbele.

Amesisitiza kuwa ushirikiano huo utakuwa mwanzo wa safari ya kuwajengea wanawake uwezo zaidi kiuchumi na kijamii.

No comments:

Post a Comment