MAAMBUKIZI YA MALARIA YASHUKA KWA ASILIMIA 30 NCHINI, VIFO VIKIPUNGUA - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Saturday, April 25, 2026

MAAMBUKIZI YA MALARIA YASHUKA KWA ASILIMIA 30 NCHINI, VIFO VIKIPUNGUA


Na Atley Kuni, WAF-Dodoma


Serikali imetangaza mafanikio makubwa katika mapambano dhidi ya ugonjwa wa Malaria nchini, huku takwimu zikionesha kupungua kwa maambukizi kwa asilimia 30 kutoka asilimia 8.1 mwaka 2022 hadi asilimia 5.7 mwaka 2025.

Kauli hiyo imetolewa na Mganga Mkuu wa Serikali Dkt. Grace Magembe Aprili, 2026 kupitia tamko la siku ya Malaria Duniani ambayo huadhimishwa Aprili 25 ya kila mwaka ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya siku hiyo.


Kwa mujibu wa taarifa ya Mganga Mkuu wa Serikali aliyoitoa kwa vyombo vya habari jijini Dodoma, Dkt. Grace Magembe, amesema idadi ya wagonjwa wa Malaria waliothibitika katika vituo vya afya imepungua kwa asilimia 53, kutoka wagonjwa milioni sita (6) mwaka 2020 hadi milioni 2.8 mwaka 2025.

"Kwa upande wa wagonjwa wanaolazwa hospitalini idadi imepungua kwa asilimia 35, huku vifo vitokanavyo na ugonjwa huo vikishuka kwa asilimia 50", amesema Dkt. Magembe. 

Dkt. Magembe amefafanua kuwa mafanikio hayo yanachangiwa na uwekezaji mkubwa wa Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa maendeleo, uliowezesha kuimarika kwa upatikanaji wa dawa na huduma za malaria bila malipo katika vituo vya afya vya umma.

Aidha, Dkt. Magembe amesema ili kuendeleza juhudi hizo, Serikali imetenga shilingi bilioni 20 kwa miaka ya fedha 2024/25 na 2025/26 kwa ajili ya unyunyiziaji wa viuadudu vya kibaiolojia kwenye mazalia ya mbu katika halmashauri zote 184 nchini.

Dkt. Magembe amesema Serikali imejipanga kutekeleza Mpango Mkakati wa Malaria wa mwaka 2026–2030 ili kuhakikisha ugonjwa huo unatokomezwa ifikapo mwaka 2030.

No comments:

Post a Comment