
Na Mwandishi Wetu, Kilimanjaro
Mahakama ya Wilaya ya Siha mkoani Kilimanjaro, Aprili 2, 2026, imewatia hatiani watumishi wawili wa Halmashauri ya Wilaya ya Siha kwa makosa ya uhujumu uchumi yanayohusisha ubadhirifu wa fedha za umma.
Washtakiwa hao ni Mohamed Khalfan Bakari, aliyekuwa Mhasibu wa Mapato, na Laurent Abiud Mgonja, aliyekuwa Mkusanya Ushuru.
Wote wamehukumiwa kutumikia kifungo cha nje cha miezi 12 pamoja na kurejesha kiasi cha shilingi milioni 12 walizobainika kujiingizia kinyume cha sheria.
Mahakama ilielezwa kuwa washtakiwa hao walifikishwa kizimbani Novemba 27, 2025, wakikabiliwa na makosa matatu likiwemo matumizi mabaya ya madaraka, ubadhirifu wa fedha na kuisababishia Serikali hasara.
Akisoma hukumu hiyo, Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Wilaya ya Siha, Mhe. Elibahati Petro, alibainisha kuwa ushahidi uliotolewa uliwatia hatiani washtakiwa hao bila kuacha shaka.
Ilidaiwa mahakamani kuwa fedha hizo zilitokana na ukusanyaji wa ushuru wa mazao katika eneo la Makiwaru, ambapo walipaswa kuziwasilisha kwenye akaunti ya Halmashauri, lakini badala yake walizitumia kwa manufaa binafsi.
Upande wa mashtaka uliwakilishwa na Wakili wa Serikali kutoka TAKUKURU, Bi. Suzan Kimaro.

No comments:
Post a Comment