Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka 2026, Ndugu Wazo Mwangonda, amezitaka Ofisi ya Halmashauri ya Wilaya ya Liwale pamoja na Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA) kuendelea kuongeza kasi ya uhamasishaji wa usajili wa Makundi Maalum kwenye Mfumo wa Kielektroniki wa Usimamizi wa Ununuzi wa Umma (NeST), ili kufikia lengo la kusajili makundi 150 kwa kila Halmashauri yatakayoweza kunufaika na fursa za zabuni zinazotengwa na Serikali.
Ndugu Mwangonda ameyasema hayo April 28, 2026 wakati akihakiki usajili wa makundi Maalum yaliyosajiliwa katika Mfumo wa NeST kwa Wilaya ya Halmashauri ya Liwale.
Amesema Serikali imeendelea kuweka mazingira rafiki ya kiuchumi kwa makundi ya Vijana, Wanawake, Wazee na Watu wenye Ulemavu kwa kutenga fursa mbalimbali za zabuni kupitia mfumo wa NeST, hivyo ni muhimu makundi hayo kujitokeza, kujisajili na kushiriki kikamilifu katika mnyororo wa ununuzi wa umma.
Ndugu Mwangonda amesisitiza kuwa usajili wa makundi hayo siyo tu fursa ya kupata zabuni, bali ni njia ya kuwawezesha wananchi kiuchumi, kuongeza ajira, kukuza kipato cha kaya na kuchochea maendeleo ya jamii kwa ujumla.
Aidha, ameipongeza Mikoa ya Pwani na Dar es Salaam pamoja na Wilaya zake kwa kufanya vizuri katika zoezi la kusajili idadi kubwa ya makundi maalum kwenye mfumo wa NeST, akieleza kuwa hatua hiyo ni mfano bora wa kuigwa na maeneo mengine nchini.
Ametoa rai kwa viongozi wa Serikali za Mitaa, taasisi za umma na wadau mbalimbali kuendelea kushirikiana katika utoaji wa elimu kwa wananchi kuhusu manufaa ya mfumo wa NeST, ili kuhakikisha makundi mengi zaidi yanafikiwa na kunufaika na fursa zilizopo.
“Uwezeshaji wa makundi maalum ni msingi wa maendeleo jumuishi. Tukiwawezesha wananchi wetu kushiriki katika uchumi rasmi kupitia zabuni za Serikali, tunajenga Taifa lenye usawa na ustawi,” amesema Ndugu Mwangonda.





No comments:
Post a Comment