SERIKALI KUENDELEA KUSHIRIKIANA NA WAWEKEZAJI WA NDANI - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Saturday, April 25, 2026

SERIKALI KUENDELEA KUSHIRIKIANA NA WAWEKEZAJI WA NDANI

NA EMMANUEL MBATILO, DAR ES SALAAM

SERIKALI imewahimiza wawekezaji wazawa kuchangamkia fursa zilizopo katika sekta ya viwanda, ikisisitiza kuwa imeendelea kuboresha na kurahisisha mazingira ya biashara ili kuongeza uwekezaji wa ndani.

Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Judith Kapinga (Mb), amesema hayo Aprili 24, 2026 jijini Dar es Salaam wakati akizindua bidhaa nne mpya za chapa ya Riviera.

Amesema Serikali ya Awamu ya Sita imejikita katika kuweka mazingira wezeshi ya biashara kwa lengo la kukuza uchumi wa viwanda na kuongeza ajira kwa Watanzania.

Aidha, Waziri Kapinga ameeleza kuwa Serikali haitofungia biashara zinazojitokeza, bali itazielekeza kufuata taratibu na viwango vinavyotakiwa ili kulinda afya ya umma na maslahi ya walaji.

“Tunaendelea kuwasisitiza wanaotaka kuingia katika sekta hii kuwa mazingira ya biashara yamerahisishwa. Endapo bidhaa haina uthibitisho, hatufungii biashara bali tunaelekeza namna sahihi ya kufuata ili kulinda afya ya Watanzania,” amesema Kapinga.

Katika hatua nyingine, Waziri Kapinga amempongeza Mkurugenzi wa Kampuni ya Lomatan, Bi. Loveness Mamuya, kwa ujasiri wa kuwekeza katika sekta ya vinywaji vikali yenye ushindani mkubwa.

Amesema uwekezaji huo ni kielelezo kuwa Watanzania wana uwezo wa kuwekeza katika sekta mbalimbali za uchumi na kushindana katika soko la ndani na nje ya nchi.

Aidha, amemhakikishia mwekezaji huyo kuwa Wizara yake itaendelea kutoa ushirikiano katika kutatua changamoto zozote zitakazojitokeza ili kuhakikisha biashara hiyo inakua na kuchangia mapato ya Serikali.

Kapinga pia amesisitiza kuwa kupitia Tume ya Ushindani (FCC), Serikali itaendelea kupambana na bidhaa haramu, hususan vinywaji visivyokidhi viwango, ili kulinda afya ya wananchi na ushindani wa haki sokoni.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Lomatan, Loveness Mamuya, amesema kampuni hiyo imeanzisha kampeni ya kupinga matumizi ya pombe feki na haramu, akieleza kuwa bidhaa hizo zinaathiri afya ya jamii na kudhoofisha nguvu kazi ya taifa.

Ametoa wito kwa Watanzania kushirikiana na Serikali kwa kutoa taarifa dhidi ya wazalishaji na wasambazaji wa vinywaji visivyo salama.

“Kama Mtanzania, hii ni brandi ya kwanza ya mwanamke Mtanzania katika ukanda wa Afrika Mashariki. Tunawaomba Watanzania, hususan wanawake, kuunga mkono jitihada hizi kwa kuhamasisha matumizi ya bidhaa salama na kupinga pombe feki,” amesema Mamuya.

Ameongeza kuwa bidhaa mpya za Riviera zimetengenezwa kwa kutumia teknolojia ya kisasa kutoka nchini Ujerumani ili kuhakikisha zinakidhi viwango vya ubora na usalama kwa watumiaji.

Bidhaa zilizozinduliwa ni Jagaboom, Lomatan Whiskey, Lomatan Gin na Lomatan Vodka.

No comments:

Post a Comment