SERIKALI YAENDELEA KUJENGA BARABARA ZA USALAMA MIPAKANI KUIMARISHA ULINZI - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Friday, April 10, 2026

SERIKALI YAENDELEA KUJENGA BARABARA ZA USALAMA MIPAKANI KUIMARISHA ULINZI


Serikali imesema inaendelea kujenga barabara za usalama mipakani kwa kiwango cha changarawe ili kuhakikisha mipaka ya nchi inakuwa salama na kuwezesha vyombo vya ulinzi na usalama kuimarisha doria.

Hayo yameelezwa na Naibu Waziri wa Ujenzi, Eng. Godfrey Kasekenya, leo Aprili 10, 2026, wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum, Mhe. Happiness Daniel Ngwando, aliyeuliza kuhusu mpango wa Serikali wa kuboresha barabara za mipakani ili kusaidia shughuli za ulinzi na usalama.

Akijibu swali hilo, Eng. Kasekenya alieleza kuwa barabara hizo ni muhimu kwa kuwa zinapita kando ya mipaka ya nchi na kusaidia vyombo vya usalama kufanya doria kwa ufanisi zaidi.

“Kwa kutambua umuhimu wa barabara hizi, Serikali inaendelea kuzijenga kwa kiwango cha changarawe ili ziweze kutumika na vyombo vya usalama kufanya doria mipakani,” amesema Kasekenya.

Amefafanua kuwa hadi sasa Serikali, kupitia TANROADS, imejenga jumla ya kilometa 1,759 za barabara za mipakani kwa kiwango cha changarawe katika mikoa mbalimbali ya mipakani.

Aidha, ujenzi wa sehemu zilizobaki unaendelea kwa awamu kulingana na upatikanaji wa fedha.

Kuhusu barabara ya Mtwara – Pachani – Tunduru (km 300), Eng. Kasekenya amesema kuwa usanifu wake tayari umekamilika, na kwa sasa Serikali inaendelea kutafuta fedha kwa ajili ya kuijenga kwa kiwango cha lami.

No comments:

Post a Comment