SERIKALI YAPONGEZWA KWA MAFANIKIO YA UWEKEZAJI KWA VIJANA BALEHE - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Thursday, April 23, 2026

SERIKALI YAPONGEZWA KWA MAFANIKIO YA UWEKEZAJI KWA VIJANA BALEHE



Na Okuly Julius, OKULY BLOG, Dodoma


Serikali imepongezwa kwa mafanikio yaliyopatikana katika utekelezaji wa Ajenda ya Taifa ya Kuwekeza katika Afya na Maendeleo ya Vijana Balehe (NAIA), huku wadau wakisisitiza haja ya kuendeleza juhudi hizo ili kukabiliana na changamoto zilizobaki.

Hayo yamebainishwa na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Amon A. Mpanju, wakati akifungua mkutano wa wadau wa kupokea matokeo ya tathmini ya mwisho ya ajenda hiyo uliofanyika Aprili 23, 2026 jijini Dodoma.

Amesema ajenda hiyo, iliyotekelezwa kuanzia mwaka 2021/22 hadi 2024/25, imelenga kuimarisha afya na maendeleo ya vijana balehe katika mikoa 13 yenye viashiria duni vya ustawi wa kundi hilo.

“Utekelezaji wa ajenda hii ulijikita katika maeneo sita muhimu, ikiwemo kuzuia maambukizi ya VVU, kutokomeza mimba za utotoni, kupambana na ukatili wa kijinsia, kuboresha lishe, kuhakikisha vijana wanamaliza elimu yao na kuwawezesha kiuchumi kupitia ujuzi,” amesema Mpanju.

Ameeleza kuwa baada ya kukamilika kwa kipindi cha utekelezaji, tathmini ya kina imefanyika ili kupima mafanikio na athari za uwekezaji huo kwa vijana, na matokeo yake sasa yanajadiliwa na wadau ili kutoa mwelekeo wa hatua zinazofuata.

Aidha, amesisitiza kuwa mafanikio yaliyopatikana si ya Serikali pekee, bali yametokana na ushirikiano wa karibu kati ya Serikali, mashirika ya kimataifa na asasi zisizo za kiserikali.

Ametaja baadhi ya miradi iliyochangia mafanikio hayo kuwa ni pamoja na AHADI, BRIGHT na VUMA, ambayo imesaidia kuboresha huduma za afya, elimu ya uzazi na kuwawezesha vijana kujitegemea.

“Ushirikiano huu umeleta matokeo chanya katika maisha ya vijana wetu, na ni muhimu kuendeleza juhudi hizi ili kuhakikisha tunafikia maendeleo endelevu,” amesisitiza.

Kwa upande wake, Dkt. Ahmad Mukuwani, aliyemuwakilisha Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, amesema ajenda hiyo imehamasisha vijana wengi kujiunga na vyuo vya ufundi (VETA) ili kupata ujuzi utakaowasaidia kujikwamua kiuchumi pamoja na kuchangia maendeleo ya taifa.

Ameongeza kuwa miongozo ya Wizara ya Elimu pia imeweka msisitizo katika suala la lishe shuleni, ambapo kwa sasa shule nyingi zimeanza kutoa chakula cha mchana kwa wanafunzi ili kuboresha afya na uwezo wao wa kujifunza.

Hata hivyo, ameeleza kuwa pamoja na mafanikio hayo, bado kuna changamoto zinazohitaji kuendelea kushughulikiwa, zikiwemo maambukizi ya VVU, mimba za utotoni na ndoa za utotoni.

“Bado kuna haja ya kuendelea kuwekeza zaidi ili kuhakikisha watoto wetu wanaepukana na changamoto hizi,” amesema.

Mkutano huo umewakutanisha wadau mbalimbali wakiwemo wawakilishi wa wizara, mashirika ya kimataifa, asasi za kiraia pamoja na vijana, kwa lengo la kujadili matokeo ya tathmini na kuweka mikakati mipya ya kuendeleza uwekezaji kwa vijana balehe nchini.




No comments:

Post a Comment