SERIKALI YARAHISISHA UPATIKANAJI WA MITAJI KUPITIA MIKOPO NAFUU - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Friday, April 10, 2026

SERIKALI YARAHISISHA UPATIKANAJI WA MITAJI KUPITIA MIKOPO NAFUU

Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Laurent Deogratius Luswetula (Mb), akijibu swali la Mbunge wa Msalala, Mhe. Mabula Johnson Magangila, aliyetaka kujua wakati ambao Serikali itaanza kutumia rasilimali zake kama dhamana ili wafanyabiashara wa Kitanzania waweze kukopesheka zaidi.

(Picha na Kitengo cha Mawasilino Serikalini, Wizara ya Fedha, Dodoma)


Na. Josephine Majura, WF, Dodoma


Serikali kupitia Wizara ya Fedha imeendelea kutekeleza mikakati ya kuimarisha uchumi wa wananchi kwa kuwezesha upatikanaji wa mitaji kupitia mikopo yenye masharti nafuu ili kuongeza uwezo wa kukopesheka kwa wafanyabiashara wadogo na wa kati, sambamba na kukuza miradi ya kiuchumi inayochangia pato la Taifa.

Hayo yameelezwa bungeni jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Laurent Deogratius Luswetula (Mb), alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Msalala, Mhe. Mabula Johnson Magangila, aliyetaka kujua lini Serikali itaanza kutumia rasilimali zake kama dhamana ili wafanyabiashara wa Kitanzania waweze kukopesheka zaidi.

Mhe. Luswetula, alisema Serikali imeweka utaratibu wa kutumia rasilimali zake kama dhamana, ambapo kupitia Benki ya NMB, wafanyabiashara wadogo na wa kati wanapatiwa mikopo kwa riba nafuu ya asilimia 7 kwa mwaka.

“Mpango huu unalenga kupunguza changamoto za kifedha zinazowakabili wajasiriamali na kuongeza ajira kwa wananchi “, alifafanua Mhe. Luswetula.

Aidha, alisema kuwa Serikali imeipatia Benki Kuu ya Tanzania jukumu la kusimamia Mifuko ya Udhamini wa Mikopo, ambayo inatoa udhamini kwa Watanzania wenye miradi yenye tija lakini wanaokabiliwa na changamoto za dhamana wakati wa kuomba mikopo.

Mhe. Luswetula, aliongeza kuwa kupitia mfumo huo, wananchi wanapata nafasi ya kufanikisha miradi yao bila kuzuiwa na vikwazo vya dhamana.

Kwa upande wa Wafanyabiashara wanaojihusisha na mauzo nje ya nchi, Mhe. Luswetula, alisema Serikali imeanzisha Mfuko wa Udhamini wa Mikopo ya Mauzo Nje ya Nchi (Export Credit Guarantee Scheme), huku wajasiriamali wadogo na wa kati wakinufaika kupitia Mfuko wa Udhamini wa Mikopo kwa Wajasiriamali Wadogo na wa Kati (SMEs Credit Guarantee Scheme).

Alisema kuwa juhudi hizo zote zinazofanywa na Serikali zina lengo la kurahisisha upatikanaji wa mikopo, kukuza miradi ya kiuchumi, na kuongeza tija katika sekta zote za uchumi.

No comments:

Post a Comment