Na Okuly Julius,OKULY BLOG,DODOMA
Shirika la Posta Tanzania (TPC) limeweka mkakati wa kukusanya jumla ya Shilingi 50,933,863,225 katika mwaka wa fedha 2026/2027, huku likipanga kutumia Shilingi 49,353,956,977 kwa ajili ya kuendesha shughuli zake na kuboresha huduma za posta nchini.
Akiwasilisha bungeni makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Waziri wa wizara hiyo, Angellah Kairuki, alisema kati ya fedha hizo, Shilingi bilioni 18 zitatumika kwa mishahara ya watumishi, Shilingi 26,853,956,977 kwa gharama za uendeshaji na Shilingi bilioni 4.5 zitatengwa kwa ajili ya miradi ya maendeleo.
Alisema katika mwaka huo wa fedha, TPC imejipanga kuboresha mfumo wa Posta Kiganjani ili kuwa jukwaa jumuishi litakalounganisha huduma zote za posta kidijitali, hatua inayolenga kuongeza ufanisi na urahisi wa huduma kwa wananchi.
Aidha, shirika hilo litatekeleza miradi 10 ya uendelezaji wa viwanja kupitia ubia (Joint Venture) katika maeneo ya kimkakati, ikiwa ni sehemu ya kuongeza mapato na thamani ya rasilimali zake.
Katika kuimarisha rasilimali watu, TPC inatarajia kuzindua na kuendesha Kituo cha Mafunzo kwa Njia ya Mtandao (TPC Virtual Academy) kitakacholenga kuboresha uongozi, ubora wa huduma na utaalamu wa watumishi wake katika sekta ya posta.
Waziri Kairuki aliongeza kuwa shirika hilo pia litasimamia uendeshaji wa vituo 32 vya huduma pamoja vitakavyoanzishwa kupitia Mradi wa Tanzania ya Kidijitali, hatua itakayorahisisha upatikanaji wa huduma mbalimbali kwa wananchi katika maeneo tofauti nchini.
Kwa upande wa usafirishaji wa vifurushi na mizigo, TPC imepanga kununua magari 12 na pikipiki 20 za umeme ili kuongeza ufanisi na kupunguza gharama za uendeshaji, sambamba na kuanzisha vituo vitano vya ukusanyaji mizigo katika maeneo ya kimkakati ikiwemo stendi za mabasi na masoko makubwa.
Aidha, shirika hilo litaendesha kampeni nne za uhamasishaji wa huduma zake, zikiwemo kampeni za kuhamasisha matumizi ya mfumo wa usafirishaji kidijitali wa SwifPack, kwa lengo la kuongeza matumizi ya huduma za posta katika mazingira ya kidijitali.
Waziri Kairuki alisisitiza kuwa utekelezaji wa mipango hiyo utaimarisha ushindani wa TPC, kuongeza mapato ya shirika na kuboresha huduma za posta ili ziendane na mahitaji ya uchumi wa kisasa unaotegemea teknolojia.


No comments:
Post a Comment