TANZANIA YAELEZA MIKAKATI YA UPATIKANAJI WA MBOLEA NA USALAMA WA CHAKULA - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Wednesday, April 15, 2026

TANZANIA YAELEZA MIKAKATI YA UPATIKANAJI WA MBOLEA NA USALAMA WA CHAKULA


Katibu Mkuu (Mipango) na Katibu Mtendaji wa Tume ya Taifa ya Mipango, Dkt. Tausi Mbaga Kida, ameshiriki katika kikao kazi maalum kilichojadili changamoto za upatikanaji wa mbolea duniani na mikakati iliyowekwa na Tanzania kuwawezesha wakulima.

Majadiliano hayo yamefanyika katika Chuo Kikuu cha George Washington nchini Marekani pembezoni mwa mfululizo wa Vikao vya Kipupwe (Spring Meetings) vinavyoendelea jijini Washington DC.

Katika mchango wake, Dkt. Kida ameeleza hali ya upatikanaji wa mbolea nchini hususani mahitaji yaliyopo huku akibainisha fursa za uwekezaji zilizopo katika uzalishaji wa Mbolea kwa kuwa kiwango kikubwa cha mbolea aina ya Urea, DAP, NPK na CAN huagizwa kutoka nje ya nchi.

Dkt Kida alieleza namna ambavyo malengo ya uzalishaji katika sekta ya kilimo yamekuwa yakifikiwa mathalani; ufanisi na uhakika wa upatikanaji wa mbegu bora na kuimarika kwa huduma za ugani.

Aidha, ameeleza mikakati ya muda mfupi, muda wa kati na muda mrefu iliyowekwa kukabiliana na athari zitokanazo na migogoro inayoendelea mashariki ya kati ambayo imeathiri kwa kiwango kikubwa upatikanaji wa mbolea nchini.

Mikakati hiyo ni kuongeza na kuboresha utunzaji wa mbolea iliyopo kwa matumizi sahihi, kutafuta vyanzo mbadala kwa ajili ya kuagiza mbolea, kuendelea na programu ya utoaji wa ruzuku katika mbolea na kuimarisha uzalishaji wa ndani.

Dr. Kida alihitimisha kwa kubainisha mafanikio ambayo Tanzania imeendelea kupata kupitia sekta ya kilimo ikiwemo matumizi mifumo ya teknolojia, tafiti zinazosaidia kuboresha matumizi ya mbolea kulingana na mahitaji ya maeneo mahsusi na utekelezaji wa Programu kama vile BBT zenye lengo la kuwainua vijana na wanawake wanaoshiriki uzalishaji wa sekta ya kilimo.


No comments:

Post a Comment