TANZANIA YAPONGEZWA KWA MCHANGO WA MADINI KWENYE PATO LA TAIFA - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Tuesday, April 28, 2026

TANZANIA YAPONGEZWA KWA MCHANGO WA MADINI KWENYE PATO LA TAIFA



📍 Nairobi, Kenya


Sekta ya Madini nchini Tanzania imeendelea kung’ara kimataifa baada ya kupongezwa kwa mchango wake mkubwa katika kukuza pato la taifa (GDP), huku nchi jirani zikieleza nia ya kujifunza mafanikio ya usimamizi wa sekta hiyo.

Wakizungumza katika Mkutano wa Kimataifa wa Uwekezaji wa Madini (Kenya Mining Investment Conference and Expo -MICE) 2026, unaofanyika jijini Nairobi kwa siku mbili 28 hadi 29 Aprili 2026 MICE 2026 Nairobi, na kuhudhuriwa na Viongozi , Wawekezaji na Wadau wa Sekta ya Madini barani Afrika, Mawaziri mbalimbali Madin wa Afrika walitambua hatua kubwa zilizopigwa na Tanzania katika kuifanya sekta ya madini kuwa mhimili wa uchumi.

Akizungumza katika mdahalo maalum wa mawaziri hao, Waziri wa Madini wa Tanzania, Mhe. Anthony Mavunde, amesema mafanikio hayo yametokana na uongozi thabiti wa Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambaye ameweka mazingira wezeshi ya uwekezaji, kuimarisha usimamizi wa rasilimali, na kusukuma mbele ajenda ya kuongeza thamani ya madini ndani ya nchi.

Awali akifungua Mkutano huo, Rais wa Kenya, Mhe. William Ruto, amezitaka nchi za Afrika Mashariki na Afrika kwa ujumla kuimarisha ushirikiano na kuunganisha nguvu katika kuongeza thamani ya rasilimali madini ili kuongeza tija na ushindani wa ukanda huo katika soko la dunia.

Akihitimisha, Waziri Mavunde amewahimiza wawekezaji wa ndani na nje ya nchi kuichangamkia Tanzania, akieleza kuwa ipo tayari kupokea uwekezaji katika maeneo ya uchimbaji, uchenjuaji na uongezaji thamani wa madini, sambamba na kuwepo kwa sera na miundombinu rafiki kwa biashara.

Katika kuonesha imani kwa Tanzania, nchi za Kenya, Somalia na Sudan Kusini zimesema zinaendelea kujifunza kutoka kwa Tanzania, hususan katika mifumo ya usimamizi, uongezaji thamani na ushirikishwaji wa wachimbaji wadogo katika uchumi wa madini.

Katika mjadala huo, Waziri wa Madini, Uchumi wa Bluu na Masuala ya Bahari Kenya, Mhe. Hassan Ali Joho, ameitaja Tanzania kuwa mfano bora wa kuigwa kikanda, akisisitiza kuwa ushindani siyo kipaumbele bali ushirikiano wa pamoja ili kukuza na kuimarisha Sekta ya Madini barani Afrika.

Naye, Waziri Waziri wa Petroli na Rasilimali Madini, Serikali ya Shirikisho ya Somalia, Mhe. Dahir Shire Mohamed, amesema kuwa nchi yake inaichukulia Tanzania ni mfano halisi katika kujenga mifumo imara ya usimamizi wa rasilimali madini na kuwa Somalia inaendelea kujifunza kutoka Tanzania.

Katika mjadala huo, viongozi wengine walioshiriki ni pamoja na Waziri wa Maendeleo ya Madini Imara wa Nigeria, Oladele Henry Alake, pamoja na Waziri wa Madini wa Sudan Kusini, Losuba Ludoru Wongo.
Kwa pamoja, mawaziri hao wamejadiliana kuendeleza ushirikiano wa kikanda, huku wakisisitiza kuwa bara la Afrika linaweza kujenga uwezo wa pamoja na kunufaika zaidi na rasilimali zake.

No comments:

Post a Comment