
Na OWM - TAMISEMI, Arusha
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OWM-TAMISEMI) Mhe. Prof. Riziki Shemdoe, ameishukuru na kuitaka taasisi ya Tanzania Road Safety Initiative (TARSI) kuendelea na utaratibu wa kutoa Mafunzo ya Usalama wa Miundombinu ya Barabara kwa wataalamu (wahandisi), wapangaji, wakandarasi, na watunga sera ili wapate ujuzi wa kuendelea kuimarisha barabara na kupunguza ajali, majeruhi na vifo vinavyoepukika.
Prof. Shemdoe ametoa wito huo leo Aprili 22, 2026 jijini Arusha wakati akifungua Mafunzo ya Usalama wa Miundombinu ya Barabara Tanzania 2026 yanayotolewa na TARSI kwa wataalamu (wahandisi), wapangaji, wakandarasi, na watunga sera katika Ukumbi wa Four Points by Sheraton Arusha, yakilenga kuwajengea uwezo wa kuimarisha miundombinu ya barabara ili kupunguza idadi ya vifo na majeruhi wa ajali za barabarani.
“Wahandisi 800 mliowapatia mafunzo hawatoshi, niwaombe muendelee kuwapatia mafunzo wahandisi wengi zaidi ili wapate maarifa na ujuzi wa kuimarisha barabara zetu za TANROADS na TARURA,” amesisitiza Prof. Shemdoe.
Sanjari na hilo, amewataka TARSI kwenda kutoa mafunzo hayo ya usalama wa miundombinu ya barabara kwenye vyuo vinavyofundisha taaluma ya uhandisi inayohusika na kubuni, kujenga na kutunza miundombinu ya msingi (Civil Engineering) na vinavyofundisha Uhandisi wa Barabara (Road Engineering) ili kuwa na mtaala utakaozalisha wataalamu watakaosaidia kuimarisha miundombinu ya barabara nchini.
Aidha, Prof. Shemdoe amewataka washiriki wa mafunzo hayo kuwa mfano wa kuigwa katika kutekeleza sheria za barabarani kwa kuzingatia alama za barabarani, huku akitoa wito kwa TARSI na washiriki wa mafunzo kuendelea kutoa elimu ya usalama barabarani kwa kwa jamii ili kukuza uelewa kwa jamii wa matumizi ya barabara na kuepuka ajali zitakazopelekea kupoteza viungo muhimu au uhai.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Tanzania Road Safety Initiative (TARSI) Mhandisi Maliki Barongo amesema kuwa, lengo kuu la mafunzo hayo ni kuimarisha namna ya kushiriki, kupanga na kuchukua hatua kuhusiana na usalama barabarani kwenye miundombinu hususani wakati wa usanifu na ujenzi wa miundombinu ya barabara, na kuongeza kuwa mafunzo hayo yameandaliwa kutokana na uhitaji halisi katika sekta ya uhandisi wa miundombinu ya barabara.







No comments:
Post a Comment