TTCL YAPANGA KUKUSANYA ZAIDI YA SHILINGI BILIONI 524, KUIMARISHA HUDUMA ZA MAWASILIANO NCHINI - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Thursday, April 30, 2026

TTCL YAPANGA KUKUSANYA ZAIDI YA SHILINGI BILIONI 524, KUIMARISHA HUDUMA ZA MAWASILIANO NCHINI


 

Na Okuly Julius,OKULY BLOG,DODOMA


Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) limepanga kukusanya jumla ya Shilingi 524,652,058,739.13 katika mwaka wa fedha 2026/2027, huku likitarajia kutumia Shilingi 482,801,024,748 kwa ajili ya kuendesha shughuli zake na kutekeleza miradi ya maendeleo.


Hayo yamesemwa leo Aprili 30, 2026 bungeni Dodoma na Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Angellah Kairuki, wakati akiwasilisha hotuba ya bajeti ya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2026/2027. 


Alisema kati ya fedha zitakazotumika, Shilingi 314,582,769,607.43 zimetengwa kwa matumizi ya kawaida na Shilingi 168,218,255,140.59 kwa ajili ya miradi ya maendeleo.


Alisema TTCL imejipanga kuongeza mapato yake ya ndani hadi kufikia Shilingi bilioni 411.7 kwa kuboresha huduma na kupanua wigo wa biashara zake katika sekta ya mawasiliano.


Katika kuboresha huduma za intaneti ya kasi, shirika hilo linatarajia kujenga maunganisho 321,000 ya huduma ya Faiba Mlangoni pamoja na kuunganisha wateja 128,800, hatua itakayorahisisha upatikanaji wa huduma za kidijitali kwa wananchi na taasisi mbalimbali.


Aidha, TTCL imeweka mpango wa kuunganisha wateja 912,700 wa huduma za mawasiliano ya simu na kuunganisha maeneo 100 ya umma na huduma ya Wi-Fi ili kuongeza upatikanaji wa intaneti katika maeneo ya kijamii.


Kwa mujibu wa Waziri Kairuki, shirika hilo pia litaunganisha vituo 20 kwenye Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano na kuendelea na ujenzi wa miundombinu hiyo ili kuiunganisha Tanzania na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), hatua itakayopanua fursa za mawasiliano na biashara kikanda.


Katika kuimarisha rasilimali watu, TTCL imepanga kutoa mafunzo kwa watumishi 340 ili kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma, pamoja na kuendesha kampeni nne za uhamasishaji ili kuongeza matumizi ya huduma zake kwa wananchi.

Waziri Kairuki alisisitiza kuwa utekelezaji wa mipango hiyo utaimarisha ushindani wa shirika hilo na kuongeza mchango wake katika maendeleo ya uchumi wa kidijitali nchini.

No comments:

Post a Comment