Wafanyabiashara wa Soko la Namanga lililopo Manispaa ya Kahama mkoani Shinyanga wameeleza kutoridhishwa na mfumo wa ukusanyaji wa ushuru wakidai kuwepo kwa tozo wanazoziita zisizo rasmi pamoja na ukosefu wa uwazi katika matumizi ya mapato yanayokusanywa sokoni hapo.
Wakizungumza katika mkutano wa kusikiliza na kutatua kero ulioandaliwa na ofisi ya Mkuu wa Wilaya katika soko hilo, wafanyabiashara wamesema wamekuwa wakikumbwa na mzigo mkubwa wa ushuru unaowadhoofisha kiuchumi, huku wakidai kuwa hakuna mrejesho wa wazi kuhusu matumizi ya fedha hizo.
Mfanyabiashara samaki katika soko hilo Irene Thomas amesema kumekuwepo kwa vikundi vinavyohusika na ukusanyaji wa mapato ambavyo havitoi taarifa za kutosha kwa wafanyabiashara, hali inayozua sintofahamu sokoni hapo.
"sisi tunalipa ushuru zaidi ya maduka makubwa wanaolipa TRA, mimi mtaji wangu laki nne mpaka tano lakini kwa mwezi ushuru nalipa laki tatu na elfu tisini nikiwa na kijana na bado sijamlipa kijana, mimi nabakiwa na nini?", amesema Irene.
Ameongeza kuwa "halafu hiyo hela ni bora ningejua inaenda serikalini, inaenda kufanya maendeleo ambapo itatengeneza barabara nami nitapita, kuliko kwenda kwenye kikundi ambacho kinakula hela ya mwananchi, kikundi hiki sidhani kama kinalipa TRA maana kinatoa risiti za makaratasi na kikundi kinaingiza zaidi ya milioni nne kwa mwezi na halmashauri inalipwa laki tano na arobaini tu".
Mfanyabiashara mwingine wa samaki amesema " sisi kwenye kikundi hicho hatumo na hatufaidiki kwa chochote mapato yao wanafaidika wenyewe ikifika mwisho wa mwaka wanapeana bahasha wenyewe sasa mimi ninachotakiwa nikilipe ni mapato ya serikali yaliyonyooka na si kulipa vikundi".
Hata hivyo, Mwenyekiti wa Soko la Namanga, Juma Jumeju, amekanusha tuhuma hizo akisema mfumo wa sasa ulianzishwa ili kurahisisha ukusanyaji wa mapato baada ya soko kukumbwa na changamoto za utulivu katika kipindi cha nyuma.
Jumeju amesema uongozi uliingia ubia na baadhi ya wafanyabiashara kuunda kikundi kilichosajiliwa kisheria kwa lengo la kuboresha mfumo wa ukusanyaji wa mapato, akibainisha kuwa kuna mkanganyiko wa uelewa kuhusu majukumu ya kikundi hicho.
“Kwa kipindi cha nyuma soko halikuwa na utulivu, ndipo tukaunda kikundi kilichosajiliwa kisheria ili kurahisisha ukusanyaji wa mapato,” amesema.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Frank Nkinda, ameeleza kuwa ni muhimu kupata uhalisia wa suala hilo kabla ya kuchukua hatua, akisema kuna haja ya kusikiliza pande zote ili kuhakikisha haki inatendeka.
Aidha, ameiagiza Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kufuatilia kwa kina malalamiko hayo ili kubaini iwapo kuna mianya ya udanganyifu au ukiukwaji wa taratibu katika ukusanyaji wa mapato sokoni hapo.
“Ninaigiza TAKUKURU kufuatilia suala hili kwa haraka ili tupate uhalisia na tufanye maamuzi sahihi ya kumaliza mgogoro huu,” amesema Nkinda.






No comments:
Post a Comment