Na WMJJWM – Dodoma
Wajumbe wa kikundi kazi cha utekelezaji wa eneo namba moja la kuimarisha uchumi wa kaya chini ya Mpango wa Taifa wa Kupinga Ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto (MTAKUWWA II) wametakiwa kuwasilisha taarifa sahihi, zenye takwimu na uchambuzi wa kina ili kusaidia maamuzi yenye tija kwa jamii.
Akifungua kikao hicho Aprili 24, 2026 katika ukumbi wa St. Gasper jijini Dodoma, Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Jinsia, Badru Abdunoor, amesema ubora wa taarifa ni msingi muhimu katika kufanikisha utekelezaji wa mpango huo.
Amesisitiza kuwa taarifa za utekelezaji zinapaswa kuakisi hali halisi ya jamii na kusaidia wadau kuelewa hatua zilizofikiwa pamoja na mwelekeo wa baadaye.
“Taarifa hizi ndizo zitakazotuongoza kujua tulipotoka, tulipo na tunakokwenda, hivyo ni lazima ziwe sahihi na zenye kuaminika.” amesema.
Aidha, ameeleza kuwa kikao hicho ni sehemu ya utekelezaji wa Mpango wa Taifa wa Kutokomeza Ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto Awamu ya Pili (MTAKUWWA II), uliozinduliwa Mei 15, 2024 kwa kipindi cha mwaka 2024/25 hadi 2028/29, ukiwa ni mwendelezo wa juhudi za Serikali katika kulinda haki na ustawi wa wanawake na watoto.
Abdunoor amebainisha kuwa kuimarisha uchumi wa kaya ni nguzo muhimu katika kupunguza vitendo vya ukatili kwani familia zenye uwezo wa kiuchumi huwa na ustahimilivu mkubwa dhidi ya changamoto za kijamii na hivyo kupunguza hatari ya ukatili.
Ameongeza kuwa kuna umuhimu wa kubuni mbinu mpya na shirikishi zitakazochochea mabadiliko chanya katika jamii, huku kikao hicho kikitoa fursa ya kutathmini mafanikio yaliyopatikana, changamoto zilizopo na kuweka mikakati madhubuti ya kuboresha utekelezaji.
Kwa upande wake, Mratibu wa MTAKUWWA kutoka Wizara hiyo, Alex Shayo, amesema mila potofu na utegemezi wa kiuchumi ni miongoni mwa visababishi vikuu vya ukatili dhidi ya wanawake na watoto huku akisisitiza umuhimu wa kuwawezesha wananchi, hususan wanawake kujitegemea kiuchumi ili kujenga jamii salama na yenye ustawi.






No comments:
Post a Comment