
Na Okuly Julius, OKULY BLOG, DODOMA
Waandaji wa ratiba za masomo nchini wamehimizwa kuandaa na kuzingatia ratiba zenye uwiano mzuri kati ya masomo ya nadharia na vitendo, hatua itakayochangia kuzalisha wataalamu wenye ujuzi stahiki, kuongeza tija katika utendaji, na kuleta mchango chanya kwa maendeleo ya Taifa.
Hayo yameelezwa na Mwenyekiti Mtendaji wa Jukwaa la Waandaji wa Ratiba za Masomo nchini, Dkt. Alfredy John Nchimbi, wakati akifunga mafunzo maalum kwa wataalamu hao.
Dkt. Nchimbi amewataka washiriki wa mafunzo hayo kujikita katika matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) katika upangaji wa ratiba, akisema teknolojia hiyo itarahisisha utendaji wa kazi na kuongeza usahihi.

“Ni vyema kwenda sambamba na mabadiliko ya teknolojia, kwani TEHAMA sasa imechukua nafasi kubwa. Hivyo, hatuna budi kuitumia ili kutengeneza ratiba kwa wakati, kwa haraka na kwa usahihi, jambo litakalosaidia wanafunzi kusoma kwa nadharia na vitendo pamoja na kupata muda wa kupumzika na kufanya shughuli nyingine,” alisema.
Aidha, alisisitiza umuhimu wa kuzingatia ratiba zinazojumuisha shughuli za malezi na makuzi ya wanafunzi ili kuhakikisha wanapata maendeleo ya kielimu na kijamii kwa pamoja.

Kwa upande wake, Mratibu wa Mafunzo hayo, Victoria Kessy, alisema uandaaji bora wa ratiba za masomo una mchango mkubwa katika kuandaa vijana wenye ujuzi wa vitendo na nadharia.
“Ratiba ikipangwa vizuri huwapa wanafunzi muda wa kutosha wa kujifunza kwa vitendo, siyo nadharia pekee. Hivyo, mpangaji ratiba ana nafasi kubwa ya kusaidia kuzalisha wahitimu wenye ujuzi kamili,” alieleza.
Naye mmoja wa washiriki wa mafunzo hayo, Moses Kaswa, alisema kuwa utaalamu wa kupanga ratiba umesaidia kwa kiasi kikubwa katika vyuo mbalimbali nchini, hasa kutokana na ongezeko la wanafunzi.
Alibainisha kuwa upangaji bora wa ratiba umewezesha wanafunzi kusoma bila mwingiliano wa vipindi na kuhakikisha walimu hawapangiwi kufundisha kwa wakati mmoja, hali inayoongeza ufanisi katika utoaji wa elimu.









No comments:
Post a Comment