Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Mhe. Dkt Rhimo Nyansaho (Mb), tarehe 24 Aprili 2026, amemtembelea na kumjulia hali Mama Maria Nyerere nyumbani kwake Msasani jijini Dar es Salaam. Katika ziara hiyo Mhe Waziri wa Ulinzi na JKT, Dkt Rhimo Nyansaho alipata fursa ya kukutana pia na familia nzima ya Marehemu Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.
Akiwa Msasani, Waziri wa Ulinzi na JKT alipata fursa ya kujadiliana mambo mbalimbali na Mama Maria Nyerere na akatumia fursa hiyo kumshukuru Mama Maria kwa mchango mkubwa wa Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere alioutoa kwa Taifa na Afrika kwa ujumla, Waziri Nyansaho akamuahidi Mama Maria Nyerere, kuwa Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan na Watanzania kwa ujumla wataendelea kumuenzi Mwalimu Nyerere daima.
Aida Mhe. Dkt Rhimo Nyansaho pamoja na kukutana na Mama Maria alipata fursa ya kukutana na wanafamilia wa Baba wa Taifa akiwemo Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Mheshimiwa Makongoro Nyerere, ambaye ni mtoto wa pili wa Mwalimu Nyerere. Wengine waliokuwepo msasani nyumbani kwa Mwalimu ni pamoja na Madaraka Nyerere, ambaye ni mtoto wa kwanza wa Mwalimu Nyerere, mtoto wa tatu wa baba wa Taifa, Magige Nyerere, pamoja na wanafamilia wengine.
Akionekana mwenye bashasha na afya njema, Mama Maria amemshukuru Waziri wa Ulinzi na JKT, Dkt Rhimo Nyansaho kwa kumtembelea na kumjulia hali, pia, akampongeza Dkt Nyansaho kwa kuteuliwa kuwa Waziri wa Ulinzi na kazi nzuri anayoifanya katika kuiongoza Wizara hiyo ya Ulinzi na JKT.
Mhe Dkt Rhimo Nyansaho akahitimisha ziara yake nyumbani kwa Baba wa Taifa kwa kumshukuru Mama Maria Nyerere kwa kumkaribisha nyumbani na akamtakia afya njema.






No comments:
Post a Comment