Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini imeipongeza Serikali kupitia Wizara ya Madini kwa hatua kubwa ilizopiga katika kuendeleza mnyororo wa thamani madini, hususan kupitia ujenzi na uimarishaji wa viwanda vya kusafisha madini ya dhahabu (Refineries) hapa nchini.
Pongezi hizo zimetolewa leo Mei 2, 2026 wakati wa majumuhisho ya ziara maalum iliyojumuisha Wajumbe wa Kamati hiyo iliyofanyika katika Mkoa wa Mwanza na Geita.
Mwenyekiti wa kamati hiyo Mhe. Subira Mgalu amesema kuwa , Wizara ya Madini imekuwa na mikakati endelevu inayowezesha Sekta ya Madini kuendelea kuwa na mchango mkubwa katika Pato la Taifa hii ni kutokana na utekelezaji wa Mipango Mikakati ikiwemo Ujenzi na uendelezaji wa viwanda vya kusafisha dhahabu, Uongezaji thamani madini , Ujenzi wa viwanda vya uchenjuaji madini na uzalishaji vipuli vinavyotumika migodini.
Mhe. Mgalu amebainisha kuwa mkakati wa wizara umesaidia Tanzania kuacha kuuza madini ghafi na badala yake kuanza kusafirisha bidhaa zilizoongezewa thamani, jambo linaloongeza Pato la Taifa na kutoa fursa mbalimbali ikiwemo fursa za ajira nchini.
Akielezea kuhusu ukuaji wa uchumi Mhe. Mgalu ameeleza kuwa Sekta ya Madini imeendelea kuratibu vyema upatikanaji wa akiba ya dhahabu kupitia Benki Kuu ya Tanzania (BoT), jambo ambalo limeimarisha sarafu ya nchi na uchumi kwa ujumla.
Kwa upande wake, Waziri wa Madini, Mhe. Anthony Mavunde, ameishukuru Kamati ya Bunge kwa ushauri wake na kuahidi kuwa Wizara itahakikisha inasaidia kuweka mazingira wezeshi ya upatikanaji wa Ithibati ya LBMA kwa viwanda husika nchini kwa kuweka mazingira ya uwezeshwaji wa mitaji na miundombinu kwa wachimbaji wadogo na wawekezaji wa ndani na nje ili kuongeza uzalishaji wa dhahabu na kuboresha na kusimamia utekelezaji bora wa sera ya uongezaji thamani nchini.
Mhe. Mavunde amefafanua kuwa kutokana na Juhudi za Rais wa Jamhuri ya Tanzania Dkt.Samia Suluhu Hassan kwasasa Tanzania ipo katika orodha ya kumi bora Barani Afrika kwa nchi zenye hifadhi ya dhahabu ambapo mpaka sasa ina tani 23.8 za hifadhi ya dhahabu na viwanda 6 vya kusafisha dhahabu.
Akiwasilisha taarifa ya mwenendo wa kiwanda cha kusafisha dhahabu cha Mkoani Mwanza (MPMR) Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) Dkt.Vence Mwase amesema kuwa, kiwanda kinatumia teknolojia ya kisasa inayowezesha kusafisha kg 480 katika kiwango cha asilimia 99.999 kwa madini ya dhahabu na kg 100 ya madini ya fedha kwa siku.
Dkt. Mwase amefafanua kuwa katika kipindi cha Oktoba 2024 hadi Machi 2026 , kiwanda kimetoa huduma ya usafishaji dhahabu jumla ya gramu 10,477,268.42 ambayo sawa na tani 10.477 kwa Benki Kuu ya Tanzania (BoT).
Afisa Mtendaji Mkuu(CEO) wa kiwanda cha kusafisha dhahabu cha Geita (GGR) Mama Sarah Masasi ameipongeza Wizara ya Madini kwa kufanya juhudi za kimkakati za kuangalia namna bora ya kuongeza kiwango cha dhahabu ghafi kupelekwa kiwandani ili kuongeza wingi wa madini ya kusafishwa kiwandani.









No comments:
Post a Comment