MBOGWE YAWAFUKUZA KAZI WATUMISHI 11 KWA UTORO, ULEVI NA UBADHIRIFU - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Saturday, May 9, 2026

MBOGWE YAWAFUKUZA KAZI WATUMISHI 11 KWA UTORO, ULEVI NA UBADHIRIFU


Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbogwe mkoani Geita limewafukuza kazi watumishi 11 wa kada mbalimbali kutokana na makosa ya utoro kazini, ubadhirifu wa fedha, ulevi pamoja na kutotii mamlaka za nidhamu.

Uamuzi huo umefikiwa katika kikao cha Baraza la Madiwani wa Halmashauri hiyo baada ya wajumbe kujigeuza Kamati na kuridhia hatua hiyo, ambapo Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mbogwe, Enock John, alitangaza rasmi uamuzi huo.

Watumishi waliofukuzwa ni pamoja na Maafisa Watendaji watano, watumishi wawili wa sekta ya afya, watatu wa kilimo na mmoja wa maendeleo ya jamii. Miongoni mwa watumishi hao, mmoja anadaiwa kuweka rehani nyaraka za Serikali ili kupata fedha za pombe.

Akizungumza katika kikao hicho, Mkuu wa Wilaya ya Mbogwe, Sakina Mohammed, aliwataka watumishi wa Serikali wilayani humo kufanya kazi kwa kuzingatia sheria, kanuni na maadili ya utumishi wa umma.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Mbogwe aliwataka watendaji wa Serikali kuwajibika ipasavyo katika kutatua kero za wananchi na kuhakikisha huduma zinatolewa kwa ufanisi.

No comments:

Post a Comment