Na Okuly Julius, OKULY BLOG, DODOMA
Jitihada za Serikali za kuhakikisha huduma za msaada wa kisheria zinawafikia wananchi wengi zaidi zimepata nguvu mpya baada ya Chama cha Mawakili wa Serikali Tanzania (TPBA) kuandaa Wakili Marathon 2026 iliyolenga kuchangisha fedha za kuendeleza utoaji wa huduma hizo nchini.
Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Zainab Katimba, amesema marathon hiyo ni sehemu ya kuunga mkono juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan za kusogeza huduma za msaada wa kisheria karibu zaidi na wananchi, hususan kupitia kampeni ya Mama Samia Legal Aid Campaign.
Akizungumza Mei 31, 2026 katika Uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma baada ya kushiriki mbio hizo zilizoendeshwa chini ya kaulimbiu ya “Msaada wa Kisheria Karibu Zaidi na Watanzania,” Katimba amesema marathon hiyo inalenga kuchangisha fedha zitakazosaidia kuimarisha utoaji wa huduma za msaada wa kisheria kwa wananchi katika maeneo mbalimbali ya nchi.
Amesema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imeweka kipaumbele katika kuhakikisha wananchi wanapata haki zao kwa urahisi kupitia huduma za msaada wa kisheria, hatua ambayo imeonekana kupitia mafanikio ya kampeni ya Mama Samia Legal Aid Campaign inayotekelezwa nchini kote.
Katimba amesema kampeni hiyo imekuwa nyenzo muhimu ya kuwafikia wananchi, hasa wale wa maeneo ya vijijini na pembezoni, kwa kuwapatia elimu ya sheria pamoja na msaada wa kisheria unaowawezesha kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili katika maisha ya kila siku.
“Lengo la Wakili Marathon ni kutafuta fedha za kuendeleza jitihada za Serikali za kuwasaidia Watanzania kupata msaada wa kisheria. Rais Samia amekuwa kinara katika kuhakikisha wananchi wanapata huduma hizi muhimu kupitia Mama Samia Legal Aid Campaign, hivyo marathon hii ni sehemu ya kuongeza nguvu katika kusogeza huduma hizo karibu zaidi na wananchi,” amesema Katimba.
Ameeleza kuwa Serikali inaamini kuwa ushirikishwaji wa wananchi kupitia shughuli za michezo unaweza kuwa chachu ya kuhamasisha maendeleo ya kijamii na kuongeza uelewa wa masuala muhimu yanayogusa maisha yao, ikiwemo haki za kisheria.
Aidha, amesisitiza kuwa Serikali itaendelea kuunga mkono mipango inayounganisha michezo, afya na huduma za kijamii kwa kuwa imeonekana kuwa njia bora ya kujenga mshikamano wa wananchi huku ikitoa fursa ya kuchangia maendeleo ya sekta mbalimbali.
“Kadiri wananchi wanavyopata elimu ya sheria ndivyo tunavyopunguza migogoro na kujenga jamii yenye amani, umoja na mshikamano,” amesema.
Hata hivyo, amewataka viongozi wa TPBA kuhakikisha Wakili Marathon inakuwa tukio la kudumu katika kalenda ya chama hicho ili kuongeza manufaa kwa wananchi na kuendeleza juhudi za utoaji wa huduma za msaada wa kisheria nchini.
Akizungumza kwa niaba ya Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mkurugenzi wa Kitengo cha Mipango, Bajeti na Ubunifu, Buji Bampebuye, amesema Wakili Marathon imekuwa jukwaa muhimu la kuwakutanisha wadau wa sekta ya sheria na wananchi katika kuhamasisha masuala ya afya pamoja na utoaji wa msaada wa kisheria.
“Marathon hii imeanzishwa kama sehemu ya mkakati wa chama kusaidia utoaji wa huduma za msaada wa kisheria nchini pamoja na kuimarisha mshikamano miongoni mwa wanachama na wadau wa sekta ya sheria,” amesema Bampebuye.
Amesema washiriki wa mashindano hayo walishindana katika makundi mbalimbali ya kilomita 5, 10 na 21, huku washindi wakikabidhiwa zawadi baada ya kumalizika kwa mashindano hayo.
Naye mwanariadha mahiri wa Tanzania, Alphonce Simbu, amewataka wananchi kuendeleza utamaduni wa kufanya mazoezi mara kwa mara ili kujikinga na magonjwa yasiyoambukiza na kuboresha afya zao.
Simbu amesema matukio ya marathoni yamekuwa na mchango mkubwa katika kuhamasisha jamii kuhusu umuhimu wa mazoezi, huku yakitoa fursa ya kuunganisha wananchi katika shughuli mbalimbali za kijamii na maendeleo.
“Ninawahamasisha Watanzania kuendelea kufanya mazoezi na kushiriki matukio ya michezo kwa sababu afya bora ndiyo msingi wa maendeleo ya mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla,” amesema Simbu.
Nao baadhi ya wadau walioshiriki katika mbio hizo wameeleza kuwa Wakili Marathon ni jukwaa muhimu la kuhamasisha upatikanaji wa haki kwa wote na kuongeza rasilimali zitakazowezesha huduma za msaada wa kisheria kuwafikia Watanzania wengi zaidi, sambamba na juhudi za Serikali za kujenga jamii yenye usawa na inayozingatia utawala wa sheria.
Wakili Marathon 2026 imekuwa ya kwanza kufanyika chini ya uratibu wa Chama cha Mawakili wa Serikali Tanzania (TPBA) na imepongezwa kwa kuunganisha michezo, afya na huduma za kisheria katika jukwaa moja.



No comments:
Post a Comment