WSDP YAFANIKISHA KUKWAMULIWA KWA MIRADI 177 YA MAJI, YAONGEZA UFADHILI WA ZAIDI YA SHILINGI TRILIONI 1.2 - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Tuesday, May 5, 2026

WSDP YAFANIKISHA KUKWAMULIWA KWA MIRADI 177 YA MAJI, YAONGEZA UFADHILI WA ZAIDI YA SHILINGI TRILIONI 1.2


Na Okuly Julius,OKULY BLOG,DODOMA


Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Maji (WSDP) imeendelea kuleta mageuzi makubwa nchini baada ya kufanikisha kukwamuliwa kwa miradi 177 ya maji vijijini iliyokuwa imesuasua, sambamba na kuongeza wigo wa ufadhili wa sekta ya maji kufikia zaidi ya Shilingi trilioni 1.2 kupitia vyanzo mbalimbali vya ndani na nje ya Serikali.


Akizungumza wakati akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Maji, Waziri wa Maji Mhe. Jumaa Aweso amesema mafanikio hayo yamepatikana kupitia usimamizi madhubuti wa WSDP ambao umeongeza ufanisi wa utekelezaji wa miradi ya maji na usafi wa mazingira nchini.


Amesema kukwamuliwa kwa miradi hiyo 177 kumeenda sambamba na kuimarika kwa miradi mikubwa ya kimkakati ikiwemo Mugango–Kiabakari–Butiama, Bunda, Same–Mwanga–Korogwe pamoja na miradi ya maji katika mikoa ya Dar es Salaam na Arusha.


Waziri Aweso amesema WSDP imeiwezesha sekta ya maji kuongeza wigo wa upatikanaji wa fedha kutoka kwa washirika wa maendeleo, taasisi za kifedha na mifuko ya kimataifa, hatua iliyosaidia kupunguza utegemezi wa bajeti ya Serikali.


Ameeleza kuwa kupitia mfumo huo, sekta ya maji imefanikiwa kuvutia na kutumia zaidi ya Shilingi trilioni 1.2 kwa ujumla kupitia michanganyiko ya fedha za ndani na nje kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maji nchini.


Katika mwaka wa fedha 2025/26, sekta ya maji imenufaika na Dola za Marekani milioni 257 kutoka Mfuko wa Mabadiliko ya Tabianchi kwa ajili ya kutekeleza miradi 15, ikiwemo Bonde la Usangu na Mradi wa Uhimilivu wa Mabadiliko ya Tabianchi katika Mto Mkondoa.


Aidha, Mamlaka za Maji zimepokea Shilingi takribani bilioni 7 kutoka Serikali ya Ujerumani kupitia mpango wa IFF-OBA kwa ajili ya kuboresha huduma za maji na usafi wa mazingira katika mikoa mbalimbali nchini.


Waziri Aweso amesema sekta ya maji imeanza kutumia hati fungani kama chanzo mbadala cha fedha, ambapo Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Tanga ilifanikiwa kuuza Hati Fungani ya Kijani yenye thamani ya Shilingi bilioni 53.12 na kukusanya Shilingi bilioni 54.72 sawa na asilimia 103 ya lengo.


Ameongeza kuwa Wizara inaendelea na maandalizi ya Hati Fungani ya Sekta ya Maji (Water Sector Bond) pamoja na Mkakati wa Ushirikishwaji wa Sekta Binafsi ili kuongeza uwekezaji katika sekta hiyo muhimu.

No comments:

Post a Comment