CBE YALETA MAGEUZI YA ELIMU KWA KOZI MPYA ZENYE MAHITAJI MAKUBWA SOKONI - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Monday, June 15, 2026

CBE YALETA MAGEUZI YA ELIMU KWA KOZI MPYA ZENYE MAHITAJI MAKUBWA SOKONI

NA EMMANUEL MBATILO, DAR ES SALAAM

CHUO Cha Elimu ya Biashara (CBE) kimepanua wigo wa fursa za elimu ya juu nchini baada ya kupata ithibati kutoka Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi (NACTVET) kwa ajili ya kuendesha programu sita mpya zitakazoanza kupokea wanafunzi katika mwaka wa masomo 2026/2027.

Akizungumza na waandishi wa habari, Mkuu wa Chuo hicho, Prof. Edda Lwoga, alisema programu hizo zimeandaliwa kwa kuzingatia mahitaji ya sasa ya uchumi, maendeleo ya sayansi na teknolojia pamoja na vipaumbele vya maendeleo ya Taifa.

Alizitaja programu mpya za ngazi ya shahada ya kwanza zinazotolewa kwa mfumo wa uanagenzi kuwa ni Bachelor of Digital Technologies Solutions Management with Apprenticeship itakayotolewa kwa ushirikiano na Mamlaka ya Serikali Mtandao (eGA), pamoja na Bachelor Degree of Banking and Credit Management with Apprenticeship itakayotolewa kwa kushirikiana na Benki ya FINCA.

Aidha, CBE imeanzisha Shahada ya Kwanza ya Business Studies and Economics with Education pamoja na shahada nne za uzamili ambazo ni Master Degree of Artificial Intelligence, Master Degree in Accounting and Finance, Master Degree of Business Administration in Entrepreneurship and Innovation na Master Degree in Marketing and Public Relations.

Prof. Lwoga alisema kuanzishwa kwa programu hizo ni sehemu ya mkakati wa chuo wa kuzalisha wataalamu wenye ujuzi unaohitajika katika uchumi wa kisasa unaotegemea teknolojia, ubunifu na maarifa.

Sambamba na hatua hiyo, dirisha la maombi ya kujiunga na programu mbalimbali zinazotolewa na CBE kwa mwaka wa masomo 2026/2027 limefunguliwa rasmi kwa waombaji kutoka ndani na nje ya Tanzania.

Ameeleza kuwa chuo kinatoa mafunzo kuanzia ngazi ya Astashahada, Stashahada, Shahada za Kwanza hadi Shahada za Umahiri katika kampasi zake za Dar es Salaam, Dodoma, Mwanza na Mbeya, hatua inayolenga kuongeza upatikanaji wa elimu bora kwa wananchi wengi zaidi.

Katika kuimarisha ushirikiano wa kimataifa, Prof. Lwoga amebainisha kuwa CBE inaendelea kutekeleza programu ya Bachelor of Business Administration (Double Degree) kwa kushirikiana na Southern West University of Finance and Economics (SWUFE) ya China, ambapo wanafunzi husoma kwa miaka miwili nchini Tanzania na miaka miwili nchini China kabla ya kuhitimu wakiwa na shahada mbili.

Amesema mfumo huo wa masomo unawapa wanafunzi fursa ya kupata uzoefu wa kimataifa, kuongeza ushindani wao katika soko la ajira na kukuza uwezo wa kufanya kazi katika mazingira ya kimataifa.

Prof. Lwoga amewahakikishia wanafunzi, wazazi na wadau wa elimu kuwa CBE ina mazingira bora ya kujifunzia, miundombinu ya kisasa ya TEHAMA, maktaba za kidijitali pamoja na wahadhiri wenye sifa na uzoefu wa kutosha.

Aidha, ameeleza kuwa ushirikiano wa chuo na sekta binafsi pamoja na taasisi mbalimbali unaendelea kutoa fursa za mafunzo kwa vitendo na ajira kwa wahitimu wake.

Amewataka vijana waliomaliza ngazi mbalimbali za elimu pamoja na wataalamu wanaotaka kujiendeleza kitaaluma kutumia fursa hiyo kujiunga na chuo hicho, akisisitiza kuwa elimu inaendelea kuwa msingi muhimu wa maendeleo ya mtu binafsi na Taifa kwa ujumla.

No comments:

Post a Comment