Na OWM – TAMISEMI, Iringa
Mkurugenzi wa Kitengo cha Michezo, Utamaduni na Sanaa kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI, Ndg. Yusuph Singo, amewataka Maafisa Michezo na Utamaduni wa mikoa na halmashauri nchini kuendelea kudumisha umoja, ushirikiano na uwajibikaji katika utekelezaji wa majukumu yao ili kuimarisha utoaji wa huduma bora kwa wananchi.
Singo ametoa wito huo Juni 24, 2026, wakati akifungua mafunzo ya upimaji wa utendaji kazi kwa Maafisa Michezo na Utamaduni wa mikoa na wilaya yaliyofanyika mkoani Iringa.
Akizungumza katika mafunzo hayo, amesema mafanikio ya taasisi yoyote yanategemea kwa kiasi kikubwa mshikamano wa watumishi wake, ushirikiano katika utendaji wa kazi na uwajibikaji wa kila mmoja katika nafasi aliyonayo.
Ameeleza kuwa katika kipindi hiki ambacho sekta mbalimbali zinaendelea kupitia mabadiliko ya kiutendaji, watumishi wanapaswa kuwa tayari kufanya kazi kwa pamoja, kubadilishana uzoefu na kusaidiana ili kufikia malengo ya taasisi kwa ufanisi zaidi.
“Majukumu yenu ni muhimu sana katika kuhakikisha wananchi wanapata huduma stahiki. Hivyo ni lazima tufanye kazi kwa umoja na ushirikiano, tukitambua kwamba mafanikio ya mmoja ni mafanikio ya taasisi nzima,” amesema Singo.
Aidha, amesisitiza kuwa mabadiliko ni sehemu ya maendeleo ya kiutendaji, hivyo ni muhimu kwa watumishi kuyapokea kwa mtazamo chanya na kushirikiana katika utekelezaji wake ili kuongeza tija, ufanisi na ubora wa huduma zinazotolewa kwa wananchi.
Singo amesema kujenga utamaduni wa kufanya kazi kwa pamoja kutasaidia kuimarisha mahusiano mema mahali pa kazi, kuongeza uwajibikaji na kuleta matokeo chanya yatakayochangia maendeleo ya jamii na Taifa kwa ujumla.
Amehitimisha kwa kuwataka maafisa hao kuendelea kushirikiana na kuzingatia maadili ya utumishi wa umma, akisisitiza kuwa umoja ndiyo msingi wa kufanikisha malengo ya taasisi na kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora kwa wakati.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chama cha Maafisa Michezo Tanzania, Bw. Kepha Elias, amewataka Maafisa Michezo na Utamaduni nchini kutekeleza majukumu yao kwa weledi, uadilifu na kujituma ili kuendelea kuimarisha maendeleo ya michezo, utamaduni na sanaa katika maeneo yao ya kazi.
Bw. Elias amesema maafisa hao wana nafasi muhimu katika kukuza vipaji, kuhamasisha ushiriki wa wananchi katika shughuli za michezo na utamaduni pamoja na kusimamia utekelezaji wa sera na miongozo ya Serikali katika sekta husika.
Ameongeza kuwa mafunzo hayo ni fursa muhimu kwa maafisa kuboresha uelewa wao kuhusu upimaji wa utendaji kazi, kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu na kuimarisha uwajibikaji katika maeneo yao ya kazi.
Mafunzo hayo yamewakutanisha Maafisa Michezo na Utamaduni kutoka mikoa na halmashauri mbalimbali nchini kwa lengo la kujengeana uwezo kuhusu upimaji wa utendaji kazi na kuimarisha utoaji wa huduma kwa wananchi kupitia sekta za michezo, utamaduni na sanaa.






No comments:
Post a Comment