
Na OKULY JULIUS, OKULY BLOG - DODOMA
WAKALA wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) umeanza maandalizi ya Mpango Kabambe wa Maji, Usafi wa Mazingira na Usafi Binafsi (District WASH Master Plan) katika wilaya 70 kati ya wilaya 128 zinazohudumiwa na wakala huo, hatua inayolenga kuimarisha uratibu wa uwekezaji na kuhakikisha miradi inatekelezwa kwa kuzingatia mahitaji halisi ya wananchi.

Akizungumza Novemba 10, 2026, jijini Dodoma, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa RUWASA, Mhandisi Amos Mtweve, amesema mpango huo utasaidia kuondoa changamoto ya utekelezaji wa miradi ya maji bila kuzingatia mipango ya sekta nyingine muhimu zinazotoa huduma kwa wananchi, zikiwemo afya na elimu.
Amesema kupitia mpango huo, RUWASA itashirikiana na wizara, halmashauri na wadau mbalimbali katika kupanga na kutekeleza miradi ya maendeleo kwa pamoja, ili kuhakikisha uwekezaji unafanyika kwa kuzingatia vipaumbele na mahitaji ya kila eneo.
Mhandisi Mtweve ameeleza kuwa awali, utekelezaji wa miradi mingi ya maji ulikuwa ukitegemea maombi yaliyotolewa na halmashauri pamoja na wabunge, hali iliyokuwa ikisababisha changamoto katika kupanga vipaumbele, kuamua maeneo ya kuanza utekelezaji na kuweka utaratibu wa kukamilisha miradi kwa awamu.
Ameongeza kuwa mpango huo utasaidia pia kuzuia mwingiliano wa miradi kati ya sekta mbalimbali, hususan pale ambapo RUWASA inapopanga kutekeleza mradi wa maji katika eneo ambalo tayari kuna mipango mingine ya maendeleo inayotekelezwa na sekta nyingine.

Kwa upande wake, Afisa Takwimu wa RUWASA, Singolile Mwamaja, amesema uandaaji wa District WASH Master Plan utahusisha ukusanyaji wa takwimu, tathmini ya mahitaji na uwekaji wa vipaumbele ili kuhakikisha mipango ya miradi ya maji na usafi wa mazingira inaendana na hali halisi ya wananchi.
Amesema hadi sasa maandalizi ya mpango huo yameanza katika wilaya sita, huku Wilaya ya Simanjiro ikiwa katika hatua za utekelezaji, ambapo kazi hiyo inatarajiwa kuchukua siku 103, kuanzia Desemba Mosi hadi Machi 30.

Naye, Meneja wa Programu wa Water for People, Mhandisi Victor Pallangyo, amesema gharama za kuandaa mpango huo hutegemea ukubwa wa kazi na mahitaji ya eneo husika.
Ametoa mfano wa Wilaya ya Mpwapwa, ambako uandaaji wa mpango huo uligharimu takribani shilingi milioni 110, huku asilimia 45 hadi 50 ya gharama hizo zikitumika katika ukusanyaji wa takwimu za awali.
Amefafanua kuwa mpango huo utaiwezesha serikali na wadau kubaini maeneo yanayohitaji uwekezaji na aina ya huduma zinazopaswa kupewa kipaumbele, zikiwemo maji, vyoo na usafi binafsi.
Aidha, amesema utasaidia kuratibu shughuli za wadau mbalimbali ili kuhakikisha rasilimali zinagawanywa kwa kuzingatia mahitaji ya maeneo husika, badala ya kujikita katika eneo moja huku maeneo mengine yakikosa huduma muhimu.
Kwa upande wake, Mratibu wa Afua za Afya na Mazingira kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI, Martha Mariki, amesema mpango huo una umuhimu mkubwa katika kuboresha huduma za afya na usafi wa mazingira katika kaya, taasisi na jamii kwa ujumla.
Amesema kuboreshwa kwa huduma hizo kutasaidia kupunguza magonjwa yanayohusiana na ukosefu wa maji safi, vyoo bora na mazingira salama.
Kikao kazi hicho cha wadau kuhusu District WASH Master Plan Concept Note na RUWASA District WASH Master Plan Guide kimefanyika kwa lengo la kujadili dhana na mwongozo wa uandaaji wa mipango hiyo katika mwaka wa fedha 2026/2027.
Katika kikao hicho, wadau wamehimizwa kutoa ushirikiano wa kitaalamu, takwimu na rasilimali ili kuhakikisha uandaaji na utekelezaji wa mipango hiyo unafanikiwa na kuchangia upatikanaji wa huduma bora za maji na usafi wa mazingira kwa wananchi.



No comments:
Post a Comment