Wakili
wa Serikali, Patrick Mwita amemuomba radhi Hakimu Mkazi Mkuu wa Kisutu
kwa kushindwa kutekeleza amri ya kumkamata mbunge wa Singida Mashariki
(Chadema), Tundu Lissu anayekabiliwa na kesi ya uchochezi pamoja na
wahariri wa gazeti la Mawio.
Wakili
Mwita alifanya hivyo jana baada ya hakimu huyo, Thomas Simba kumuhoji
sababu za kushindwa kutekeleza amri hiyo wakati hati ya kumkamata
ilitolewa Novemba 3, 2016 na wakili huyo kuisaini. “Kwa nini hamkumkamata” Si mlikuwa na wajibu wa kumkamata? Mnamuogopa?”alihoji hakimu huyo.
Hata
hivyo, pamoja na kuomba radhi hiyo mahakama imechukua hati ya kusafiria
ya Lissu ili kudhibiti safari zake nje ya nchi kwa kuwa amekuwa
akisafiri bila kuitaarifu mahakama.
Katika
kesi hiyo, Lissu na watu wengine watatu wameshtakiwa kwa makosa matano
ya uchocheza kutokana na habari iliyochapishwa na gazeti la Mawio kuhusu
hali ya kisiasa Zanzibar.
Hakimu Simba ameahirisha kesi hiyo hadi Novemba 28, 2016 na washtakiwa wote wapo nje kwa dhamana.
Kabla ya uamuzi huo, Wakili Mwita alisema jana ilikuwa siku ya kesi hiyo kutajwa na kwamba upelelezi unakaribia kukamilika.
Kuhusu
madai ya kudharau mahakama Wakili Peter Kibatala anayemwakilisha Lissu
aliiambia mahakama kuwa mteja wake yupo mahakamani, hivyo ametii amri ya
mahakama na kwamba jukumu la dhamana ni kuhakikisha mshtakiwa anakuwapo
mahakamani wakati wa kesi yake na kwamba uwepo wake ni kutii masharti
ya dhamana.
Hata
hivyo, Wakili Mwita alidai kuwa kitendo cha Lissu kutofika mahakamani
mara mbili mfululizo ni kama kuonyesha dharau kwa mahakama hiyo.
Mwita
alidai kuwa Lissu ni mwanataaluma wa sheria na anafahamu taratibu za
kufuatwa kama hafiki mahakamani na kwamba mdhamini si mbadala wa
mshtakiwa mahakamani.
“Alipaswa
kuandika barua kuitaarifu mahakama hii kama wakili kuwa ana kesi ya
uchaguzi anayoiendesha Bunda na kuambatanisha na samansi ama orodha ya
kesi. Tunaomba mahakama iheshimiwe na jukumu la kumfutia dhamana ama
kutokumfutia dhamana Lissu bado lipo mikononi mwako mheshimiwa,” alieleza wakili huyo wa Serikali.
Akizungumzia
hoja hizo, Hakimu Simba alisema Lissu ni wakili maarufu, msomi na
anajua taratibu zote za mahakama, lakini wadhamini wake wanababaika,
hivyo alimtaka aeleze sababu za kwenda Ujerumani bila kutoa taarifa
mahakamani.
Lissu
alijibu kuwa hakuwa na nia ya kuidharau mahakama, wala kuikimbia kesi
inayomkabili bali alikwenda Ujerumani katika mazingira ya dharura.
Hakimu
Simba alimwambia mahakama inafahamu kesi za uchaguzi na maelekezo yake,
hivyo ikamuuliza sababu za kutotoa taarifa wakati alipokwenda
kushughulikia kesi ya Bunda
“Nilipopata
taarifa ya kwenda kuiendesha kesi hiyo ilikuwa ni siku moja baada ya
kutoka nchini Ujerumani na kwamba niliandika barua ya kuitaarifu
mahakama na nilituma iletwe mahakamani kupitia wasaidizi wangu,”alisema Lissu.
Lakini Hakimu Simba alisema: “Hakuna
barua iliyotufikia. Usituingize katika migogoro kutokana na nafasi yako
katika jamii ya mwanasheria. Hatukuogopi labda upande wa mashtaka ndio
wamekuogopa.
“Tunataka
kufuata mfumo, hatutakuogopa na wala hatutakuonea. Hapa naona upande wa
mashtaka wanapiga blaa blaa, tuelewane tunaichukua hati yako ya
kusafiria ili ukitaka kusafiri tujue.”
No comments:
Post a Comment