WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ametembelea kiwanda cha sukari cha TPC kilichopo Arusha Chini, wilayani Moshi, mkoani Kilimanjaro na kukagua baadhi ya miundombinu ya kiwanda pamoja na mashamba.
Akiwa
kiwandani hapo, Waziri Mkuu alielezwa kwamba hivi sasa msimu wa
uzalishaji umefungwa na kiwanda kinafanyiwa matengenezo ambapo
alishuhudia baadhi ya mitambo ikiwa imefunguliwa na kufanyiwa ukarabati.
Akitoa
taarifa juu ya matengenezo hayo mwishoni mwa wiki, Meneja wa Kiwanda
hicho, Bw. Pascal Petiot alimweleza Waziri Mkuu kwamba kiwanda hicho
kimefungwa kwa zaidi ya wiki sita ili kujiandaa na msimu ujao wa
uzalishaji ambao uko karibuni kuanza.
“Hivi
sasa ni kipindi cha mvua, tumefunga msimu wa uzalishaji na tunaendelea
na ukarabati wa mitambo ili kujiandaa na msimu ujao. Kila mwaka ni
lazima tufunge msimu kwa kipindi kifupi, ili kufanya ukarabati kama
huu,” alisema.
Akiwa
kiwandani hapo, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alikuta mafundi wakifanya
matengenezo katika sehemu mbalimbali za kiwanda. Hata hivyo, alionyeshwa
mtambo wa kuzalisha umeme wa kiwanda hicho (boiler) ambao unatumia
mabaki ya miwa yaliyokwisha kamuliwa juisi (bagasse) ambayo huchomwa na
kuchemsha maji ili kupata mvuke unaosukuma jenereta.
“Tunatumia
mabaki ya miwa badala ya kuni, joto linalozalishwa linafikia nyuzijoto
450 na kuweza kuzalisha megawati 17.5 wakati kiwanda kikiwa kinafanya
kazi. Matumizi yetu kwa ajili ya kiwanda, makazi ya watumishi na vijiji
vya jirani yanafikia megawati 12, na tunawauzia TANESCO megawati 4
ambazo wanaziingiza kwenye gridi ya Taifa,” alisema Bw. Jaffari Ali
Omari ambaye ni Afisa Utawala Mtendaji.
Bw.
Omari alimweleza Waziri Mkuu kwamba umeme unaozalishwa na kiwanda hicho
ni mwingi kuliko unaozalishwa na mabwawa ya Hale na Nyumba ya Mungu
yakijumuishwa kwa pamoja. “Hale inazalisha megawati nane na Nyumba ya
Mungu inazalisha megawati tatu,” alisema.
Kwa
upande wake, Mtendaji Mkuu wa kiwanda hicho, Bw. Robert Baissac alisema
uzalishaji wa sukari kwenye kiwanda hicho umepanda kwa asilimia zaidi
ya 200 tangu wachukue kiwanda hicho mwaka 2000.
Alisema
wakati wanaanza, kiwanda kilikuwa na uwezo wa kuzalisha tani 36,000 kwa
mwaka na wakati wanakinunua walitakiwa kuongeza uzalishaji kwa asilimia
100 kwa kufikisha tani 72,000 za sukari.
“Tuliweza kuvuka lengo hilo tangu mwaka 2007 na hivi sasa tumeweza kuzalisha tani 111,800 katika msimu uliopita,” alisema.
“Tunatumia
mbegu bora zilizofanyiwa utafiti na majaribio hapa hapa kiwandani.
Tunatumia mbolea na njia za umwagiliaji ili kuhakikisha hadhi ya miwa
yetu ni ya kuridhisha, na inayoweza kutupatia kiwango kikubwa cha
sukari,” alisema.
Akitoa
maoni ya jumla, Waziri Mkuu aliwataka wafanyakazi wa kiwanda hicho
wafanye kazi kwa bidii na kujituma na kuhakikisha wanaongeza tija katika
uzalishaji wao.
“Msisitizo wa Serikali ni kuwasihi Watanzania tubadilike, tuchape kazi ili tuweze kuongeza tija mahali pa kazi,” alisema Waziri Mkuu.
Alikuwa
akijibu hoja ya Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyakazi kiwandani hapo
(TASIWU), Bw. Bilal Omar Mchomvu ambaye aliomba Serikali iangalie
uwezekano wa kuondoa makato ya kodi kwenye bonasi na overtime
wanazolipwa na kiwanda hicho.
Kuhusu
haki za wafanyakazi kiwandani hapo, Bw. Mchomvu alimweleza Waziri Mkuu
kwamba chama cha wafanyakazi kina mahusiano mazuri na menejimenti ya
kiwanda na kwamba kila miezi mitatu wanakutana na wafanyakazi hao kama
sheria inavyotaka.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMATANO, MEI 3, 2017.
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMATANO, MEI 3, 2017.
No comments:
Post a Comment