Mbunge wa Rombo (Chadema), Joseph
Selasini ameomba Mbunge wa Ulanga (CCM), Goodluck Mlinga ahusishwe
katika uchunguzi wa tukio la kushambuliwa Tundu Lissu.
Selasini ametoa ombi hilo bungeni mjini
Dodoma jana Alhamisi Novemba 9,2017 jioni akichangia mjadala wa
mapendekezo ya mpango wa maendeleo wa Taifa kwa mwaka 2018/19 na
mwongozo wa maandalizi ya mpango na bajeti kwa mwaka 2018/19.
Mbunge huyo wa Rombo akichangia alisema
mbunge huyo alishahusishwa na mauaji ya mpenzi wa mpenzi wake, hivyo ni
vyema akahusika na uchunguzi huo.
Baada ya mbunge huyo kueleza hayo,
Mlinga aliomba kwa Spika ampe taarifa Selasini akisema katika kipindi
cha uhai wake hajawahi kuhusishwa na mauaji.
“Ninamheshimu sana mheshimiwa Selasini.
Tangu nizaliwe sijawahi kuhusishwa na kifo cha mpenzi wa rafiki yangu
namuomba alete ushahidi katika Bunge hili ni nani alinihusisha,” alisema
Mlinga.
Mwenyekiti wa Bunge, Nagma Giga
alimuuliza Selasini kama anapokea taarifa hiyo lakini mbunge huyo
aliendelea kushikilia msimamo wake akisema suala hilo liliandikwa katika
gazeti la Dira.
“Nimemsikia na huo ni mkuki kwa nguruwe
lakini kwa binadamu ni mchungu. Gazeti la Dira liliandika vizuri sana
kuwa mpenzi wako alikusaliti. Wewe na kundi la vijana wenzako mkaenda
kumuua. Liliripotiwa polisi na limeripotiwa kwenye magazeti na hujawahi
kukanusha hadi leo,” alisema.
Selasini alisema, “Ningeiomba Serikali
katika uchunguzi wa nani waliohusika kutaka kudhulumu maisha ya Tundu
Lissu, huyu ambaye ameshatajwa kwamba alihusishwa na mauaji uchunguzi
uanzie kwake,” alisema.
Mbunge huyo wa Rombo alisema asubuhi
wakati Mlinga alipoomba mwongozo wa Spika, mwongozo wake ulijaa kejeli
na kumhusisha Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe
na mauaji ya albino.
Katika mwongozo huo, Mlinga alihoji
hatua ya Mbowe kutaka wachunguzi wa kimataifa kuchunguza tukio la Lissu
aliyejeruhiwa kwa risasi Septemba 7 mjini Dodoma na kuhoji ni kwa nini
hakuwahi kutaka wachunguzi hao katika mauaji ya albino.
Mlinga alisema kwa kuwa kuna taarifa
kuwa wapo wanasiasa wanahusika na mauaji ya albino basi Mbowe naye ni
mhusika na pia akasema ni kwa nini hakuhoji mauaji ya watu wa Kibiti na
Rufiji.
Hata hivyo, Spika Job Ndugai alisema
kwake haoni kama kuna mwongozo na kuelekeza shughuli za Bunge ziendelee
kwa wachangiaji kuanza kuchangia mpango huo.
Asubuhi katika kipindi cha maswali ya
papo kwa hapo kwa Waziri Mkuu, Mbowe alimuomba waziri mkuu akubali
wachunguzi wa kimataifa waje nchini kuchunguza tukio la kushambuliwa
Lissu ambaye anaendelea na matibabu katika Hospitali ya Nairobi nchini
Kenya.
Akijibu swali hilo, Waziri Mkuu, Kassim
Majaliwa alisema bado vyombo vya kiuchunguzi nchini havijashindwa
kuchunguza tukio hilo na akawahakikishia Watanzania kuwa uchunguzi
unaendelea.
No comments:
Post a Comment