UMEME KUTOKA KITUO CHA KUZALISHA UMEME KWA KUTUMIA GESI ASILIA KINYEREZI KUTUMIKA KUENDESHA TRENI YA MWENDOKASI - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Monday, March 28, 2022

UMEME KUTOKA KITUO CHA KUZALISHA UMEME KWA KUTUMIA GESI ASILIA KINYEREZI KUTUMIKA KUENDESHA TRENI YA MWENDOKASI

Naibu Waziri wa Nishati, Wakili Stephen Byabato akiongea na waandishi wa habari mara baada ya kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji na Mitaji ya Umma kufanya ziara katika kituo cha kuzalisha umeme kwa kutumia gesi asilia ambapo amesema umeme kutoka katika kituo hicho ndio utatumika kuendesha treni ya umeme. 

Na Mwandishi wetu Dar es salaam 

Reli ya Kisasa (SGR) ambayo ujenzi wake unaendelea hapa nchini ni reli ya kisasa na ya kwanza kwa Afrika Mashariki na kati itakayokuwa na uwezo wa kupitisha treni zitakazoendeshwa kwa nishati ya umeme na yenye mwendo kasi usiopungua kilometa 160 kwa saa.

Katika kufanikisha hilo, Wizara ya Nishati kupitia Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) limeweka wazi mikakati yake katika kuhakikisha treni hiyo umeme itafanya kazi zake kwa ufanisi bila changamoto yoyote kutoka katika upatikanaji wa nishati ya umeme katika kuendesha treni. 

Hayo yamesemwa leo Jumatatu Machi 28, 2022 jijini Dar es Salaam na Naibu Waziri wa Nishati, Wakili Stephen Byabato akiongea na waandishi wa habari mara baada ya kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji na Mitaji ya Umma kufanya ziara katika kituo cha kuzalisha umeme kwa kutumia gesi asilia ambapo amesema umeme kutoka katika kituo hicho ndio utatumika kuendesha treni ya umeme. 

Naibu Waziri Byabato ameongeza kuwa, njia maalumu ya kusafirisha umeme itajengwa kutoka katika kituo cha Kinyerezi kwenda Kingolwira mjini Morogoro na kitakuwa na uwezo wa kilovolti 220 na hivyo hakutakuwa na hitilafu ya kukatika kwa umeme katika shughuli zote za uendeshaji wa treni ya umeme mara tu itakapoanz kazi. 

Akielezea utekelezaji wa miradi ya upanuzi katika kituo cha Kinyerezi Naibu Waziri huyo amesema, miradi hiyo inatekelezwa kwa fedha za ndani, na wao kama wizara tayari wameshapokea fedha zote hivyo imani yao ni kwamba miradi itakamilika kwa wakati bila kisingizio. 

"Miradi ya upanuzi katika kituo cha kuzalisha umeme Kinyerezi inatekelezwa kwa fedha za ndani kwa asilimia 100, na hadi hivi sasa fedha za kukamilisha mradi wa upanuzi wa Kinyerezi 1 (Kinyerezi 1 Extension) kiasi cha dola za kimarekani milioni 52 tayari zipo mkononi mwetu, hivyo hatutarajii kuchelewa au kutokamilika mradi kwa wakati kwa kuwa fedha tayari zipo" alisema Byabato 

Mhe. Byabato ameendelea kwa kusema kuwa, kufikia Mwezi ujao (mwezi Aprili) mashine mbili katika mradi wa upanuzi wa Kinyerezi 1 (Kinyerezi 1 Extension) zitawashwa ili kuanza kuzalisha umeme, na mashine nyingine mbili kuwashwa mwezi Agosti, mwaka huu.

"Mwezi Aprili, mwaka huu tutawasha mashine mbili katika mradi wa Kinyerezi 1 Extension, mwezi wa Agosti tutawasha mashine nyingine mbili, mwezi Septemba, Oktoba na Novemba tutakuwa tunakamilisha utekelezaji wa miradi ya kutoa umeme hapa Kinyerezi kupeleka maeneo mengine" alisisitiza Byabato

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge Uwekezaji na Mitaji ya Umma (PIC), Jerry Slaa mara baada ya kutembelea kituo hicho amesema, kazi za utekelezaji wa miradi katika kituo cha kuzalisha umeme kwa kutumia gesi asilia cha Kinyerezi inaendelea vizuri, na kuweka kielelezo cha kuonesha ni namna gani TANESCO ilivyojipanga katika kuhakikisha kwamba upatikanaji wa umeme nchini unakuwa ni wa uhakika.

"Kazi zinaendelea kufanyika vizuri, na tunaona namna TANESCO walivyojipanga kuhakikisha upatikanaji wa umeme unakuwa ni wa uhakika nchini" alisema Jerry Silaa na kuongeza 

"Sisi kama kamati tumekuja kuwasikiliza wanaokisimamia kituo cha kuzalisha umeme cha Kinyerezi na hatimaye kuishauri serikali ili waweze kufanya yale ambayo tunaamini wakifanya, Tanzania itakuwa na umeme wa uhakika kwa matumizi yote ikiwemo ya viwanda na majumbani"

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Maharage Chande ameeleza kuwa, wao kama Shirika wamejiwekea lengo la kuzalisha megawati 5000 ifikapo mwaka 2025 na megawati 18,000 ifikapo mwaka 2040 hayo yote ikiwa ni katika kuboresha zaidi huduma ya upatikanaji wa umeme kwa matumizi mbalimbali.

Kando na hayo, Bw. Chande amesema kuanzia mwezi Mei, mwaka huu watakuwa na huduma ya kidijitali, huduma ambayo itakwenda kumaliza changamoto ya upatikanaji wa namba ya malipo (control number) na vishoka (mafundi wa umeme ambao hujifanya ni waajiriwa wa TANESCO).

"Mwezi Mei, 2022 tutaleta huduma ya kuunga umeme kiganjani kupitia simu, tovuti. Lengo la kuleta huduma hii ni kuondoa vishoka na changamoto ya upatikanaji wa namba ya malipo (control number)" alisisitiza Chande

Kituo cha kuzalisha umeme kwa kutumia gesi asilia cha Kinyerezi kinajumuisha mradi wa Kinyerezi 1 unaozalisha megawati 150, Kinyerezi ll unaozalisha megawati 240 pamoja na Mradi wa Upanuzi wa Kinyerezi 1 (Kinyerezi 1 Extension) ambao unatarajiwa kuzalisha megawati 185 na kuziingiza katika grid ya Taifa ifikapo mwezi Agosti, mwaka huu

No comments:

Post a Comment