Na Okuly Julius-Dodoma
SERIKALI kupitia Wizara ya Maji kwa kushirikiana na Mamlaka ya Majisafi na usafi wa Mazingira Dodoma (DUWASA) ipo katika hatua za mwisho za kumpata Mkandarasi Mshauri kwa ajili ya mradi wa uboreshaji wa huduma ya majitaka jijini Dodoma.
Mradi huo wenye thamani ya Bilion 161 umefadhiliwa na Serikali ya Korea kupitia mkopo wa Masharti nafuu unaolenga kuhudumia kata 11 na kuboresha mtandao uliopo katika kata 14.
Akizungumza na waandishi wa habari Julai 25,2022 jijini Dodoma Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Majisafi na usafi wa Mazingira Dodoma (DUWASA) Mhandisi Aron Joseph wakati akielezea utekelezaji wa shughuli mbalimbali za mamlaka hiyo na mwelekeo wa utekelezaji wa bajeti kwa mwaka wa fedha 2022/23 amesema kuwa Mradi huo utaweza kutibu majitaka lita milioni 20 kwa siku,ujenzi wa mabwa 16 eneo la Nzuguni,Utaongeza mtandao wa majitaka usiopungua kilomita 250,utaunganisha wateja wasiopungua 6,000 na
Utaongeza huduma ya usafi wa Mazingira kutoka asilimia 20 hadi 45.
Pia Mhandisi Aron amesema kuwa Mradi wa Majitaka na uboreshaji huduma ya Majisafi kwenye Mji wa Serikali ambao unashughulikiwa na Serikali kupitia Wizara ya Maji kwa kushirikiana na DUWASA ipo katika hatua za mwisho kusaini mkataba na Mhandisi Mshauri ukitarajiwa kugharimu takribani shilingi za kitanzania Bilioni 94, ambazo zimeshatengwa na Serikali Kuu.
"Dodoma kwa sasa imekuwa sana tofauti na miaka ya nyuma na ndio maana sisi kama DUWASA tunafanya kila jitihada za kuboresha miundombinu ya maji safi na majitaka kwa sababu ukiangalia hata idadi ya majengo na watu imeongezeka na kila nyumba inahitaji majisafi na miundombinu bora ya majitaka na ndio maana tunapambana kutaka kutekeleza Miradi hiyo"Amesema Mhandisi Aron
Pia amewataka wananchi wa mkoa wa Dodoma kulinda na kuhifadhi miondombinu ya maji ikiwemo kuacha tabia ya kutupa taka ngumu kwenye mabomba yanayopitisha Majitaka kwani wanasababisha kuziba na badala yake yanapasuka hivyo kusababisha uchafuzi wa mazingira.
Akizungumzia suala la Upatikanaji wa maji safi Mkurugenzi huyo amesema kuwa kwa makadirio yaliyopo Mamlaka hiyo inahudumia zaidi ya wakazi - 500,000 ambapo wanaopata Majisafi ni asilimia themanini na mbili (82%).
"Niwaambie tu ndugu waandishi kwa sasa tuna wakazi laki tano 500000 tunaowahudumia na Mahitaji ya maji - lita milioni 133 kwa siku (Mwaka 2022) na yataongezeka hadi lita milioni 204 kwa siku (mwaka 2036)" Ameongeza Mhandisi Aron
Katika hatua nyingine Mhandisi Aron amewataka wateja wa Mamlaka hiyo kulipa Ankara zao mapema ili kuepuka usumbufu wa kusitishiwa huduma na wakumbuke kuhakiki bili zao pindi wanapopata ujumbe wa usomaji wa mita zao.
"Wateja wetu jitahidini kulipa Ankara (bill) zenu za Maji usisubiri mpaka deni liwe kubwa alafu ndio uje kulipa baada ya kukatiwa maji hivyo unaatutafutia lawama tu alafu kingine mmekuwa wazito sana kuja kuhakiki bili zenu pindi mnapopata ujumbe mfupi ambao umekuwa unatumwa katika simu zenu ninawaomba mjitahidi kujenga tabia ya kuhakiki kabla hujalipa ili kujiridhisha ni kweli bili uliyopewa ni sawa na matumizi yako? " Amesisitiza Mhandisi Aron
Kwa upande wake Msemaji Mkuu wa Serikali na Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Habari maelezo Gerson Msigwa ametoa pongezi kwa mamlaka hiyo akisema kuwa wamejitahidi kuboresha upatikanaji wa majisafi ukizingatia na kasi ya ukuaji wa mkoa wa Dodoma.
"Niwapongeze tu DUWASA kwani mmeonesha mfano mzuri kivitendo kwani pamoja na serikali kuhamia Dodoma kikamilifu bado mmesimama imara na mpaka sasa mnaendelea kuhakikisha huduma ya maji katika jiji la Dodoma inaboreshwa kulingana na idadi kubwa ya watu iliyoongezeka kwa kipindi kifupi" Amesema Gerson Msigwa
Msigwa ameongeza kuwa kumtua mama ndoo kichwani ni jukumu ambalo Mhe.Rais Samia amelibeba hivyo kupitia mamlaka mbalimbali za majisafi na usafi wa mazingira kutoka mikoa yote imsaidie Mhe.Rais kutimiza adhma hiyo.
Kwa sasa kuna miradi mikubwa ya maji ambayo yakikamilika yatasaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza adha ya maji katika mikoa ya Dodoma,Mwanza na Mbeya ambapo kwa Dodoma kuna mradi wa kutoa maji kutoka Mtera na lile la Bwawa la Farkwa ambapo miradi hiyo ikikamilika tatizo la maji litakuwa limepungua kwa kiasi kikubwa.
No comments:
Post a Comment