Na Okuly Julius Dodoma
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Samia Suluhu Hassan amewataka waendesha bodaboda na bajaji nchini kutambua kuwa wao ni wasafirishaji wa taifa hivyo watumie nafasi hiyo kufanya mambo mema kwa jamii ikiwemo kuhamasisha zoezi la sensa ya watu na makazi na kuacha ukwapuaji wa mizigo ya watu.
Rais Samia ameyasema hayo kwa njia ya Simu mara baada ya kupiga simu katika kongamano la waendesha bodaboda na bajaji uliofanyika jijini Dodoma Julai 24,2022 na kusema kuwa bodaboda ni kundi muhimu sana kwa jamii ya kitanzania.
"Tuache tabia ya kukwapuakwapua mizigo ya watu,msitumie bodaboda vibaya ninyi ni watu muhimu sana ninawaomba sana katika hilo muwe walinzi wa amani taifa linawategemea sana" Mhe.Rais Samia
Na kuongeza " Nendeni mkahamasishe zoezi la sensa la watu na makazi kwa sababu tukijua idadi ya watu tutaweza kuwasaidia kwa pamoja na maendeleo ya taifa yataonekana kwa ujumla nendeni mkahamasishe watu kushiriki zoezi hilo"
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Anthony Mtaka amesema kuwa washiriki wa kongamano hilo limejumuisha madereva bodaboda 4,000 wakiwemo viongozi wao kutoka Mikoa yote nchini.
Amesema wawakilishi hao ni wawili kutoka kila mkoa, wawakilishi 30 kutoka katika kila wilaya za Mkoa wa Dodoma na Halmashauri ya Wilaya ya Dodoma 2000.
Mtaka Amesema kuwa kwa makadirio ya harak Dodoma Mjini ina bajaji na pikipiki takribani 10,000 ambazo zimeshikilia vijana wengi ambao wamejiajiri hivyo inaonesha ni jinsi gani kundi hilo lilivyo katika taifa hili.
Pia ameongeza kuwa simu aliyopiga Rais ni maelekezo hivyo kama wasaidizi wake ni kuhakikisha wanayafanyia kazi ili kuboresha utendaji kazi wa kundi hilo
"Simu aliyopiga Mh.Rais ni maelekezo hivyo aliyoyasema tumeyachukua na tutayatendea kazi ila nawaambia tu Rais anawapenda sana na nyinyi msimuangushe fanyeni mambo yanayopendeza katika jamii na msikubali kutumika vibayaa katika matukio ya kihalifu na kama kuna Changamoto zote tumezipokea na kila changamoto itajibiwa kwa aandishi," amesema Mtaka
Pia amewataka kuheshimu kazi ya udereva wa bodaboda na bajaji kwani imekuwa ikifanywa na watu wenye sifa mbalimbali na wengine ni kuna vijana waliohitimu Chuo Kikuu.
Ameyataka mashirika mbalimbali yaliyoshiriki katika kongamano hilo likiwemo Shirika la Hifadhi ya Jamii (NSSF), Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), Wakala wa Barabara Mijini na Vijijini (Tarura) na mabenki ikiwemo benki ya NMB na NBC kushirikiana vyema na kundi hilo kivitendo kama kuna namna ya kuwasaidia kuwa gharama nafuu waweke utaratibu wa kufanya hivyo.
Naye Mtakwimu Mkuu wa Serikali Dk Albina Chuwa amesema makarani wa sensa ni vijana wanaofahamika kwani wanatoka kwenye maeneo wanayoishi na wataweka utaratibu wa kutumia kundi la maofisa usafirishaji kupitia mkakati wa kuhamasisha sensa.
Adha,Dkt.Chuwa ameongeza kuwa kwa sensa hii hakutakuwa na utaratibu wa makarani kupita katika majumba ya watu usiku wa manane hivyo sensa ya watu na makazi itafanyika muda mzuri sio usiku hivyo akawataka Madereva bajaji na bodaboda kusaidia katika kuhamasisha jamii juu ya zoezi hilo
Kwa upandewa Mkuu wa kikosi cha usalama barabarani Mkoa wa Dodoma, Boniface Mbao amesema kuwa kero nyingi zilizowasilishwa katika mkutano huo wamezichukua kama jeshi la polisi na watazifanyia kazi ikiwemo baadhi ya makosa ya kimaadili yanayohusisha Askari wa kikosi cha usalama barabarani.
"Kuna mmoja hapa ameeleza kuwa alikamatwa na Polisi na akapigwa yeye pamoja na abiria wake faini kama hilo limetokea hayo sio maelekezo ya Jeshi la Polisi, tutalifanyia kazi jambo hili na kuchukua hatua," amesema
Pia ameelezea sababu inayofanya madereva bodaboda na bajaji kutakuwa kulipa faini ya papo kwa papo ni kwamba vyombo hivyo havijaingizwa kwenye mfumo wa posi na vingi havina usajili wa moja kwa moja zina sajili za kampuni.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Ardhini na nchi kavu (LATRA) ,Habibu Suluo akizungumza kwa njia ya simu ametolea ufafanuzibaadhi ya changamoto zilizotolewa na madereva haokuhusu kutozwa faini kubwa na kusema kuwa kwa sasa marekebisho yamefanyika faini zitakuwa ni Sh 25,000 kwa madereva watakaokiri makosa bila kufikishwa mahakamani na makosa yatayokwenda mahakamani faini ni Sh 30,000 hadi 50,000 badala ya zile faini za awali ya Sh 50,000 hadi 100,000.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Jabir Shekimweri amesema kuwa katika maboresho ya Jeshi l Polisi wajitahidi kufunga mifumo ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) Ili matukio ya kihalifu,makosa ya uporaji yaweze kufahamika na wanaofanya hayo wajulikane.
No comments:
Post a Comment