Rais Samia Azindua Hospitali ya Rufaa Njombe - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Tuesday, August 9, 2022

Rais Samia Azindua Hospitali ya Rufaa Njombe


Na Immaculate Makilika - MAELEZO, Njombe

Rais Samia Suluhu Hassan amezindua Hospitali ya Rufaa Njombe ambayo ujenzi wake ulianza mwaka 2016 na kugharimu shilingi bilioni 27.5 yenye majengo 15 kwa lengo kuwapatia wananchi wa Njombe na mikoa ya jirani huduma bora za matibabu.

Akizungumza leo mara baada ya kuzindua hospitali hiyo, Rais Samia amesema kuwa Serikali imeendelea kusogeza karibu huduma kwa wananchi ikiwa ni utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi.

"Niwahakikishie yale yote tuliyoahidi Serikali inakwenda kutekeleza ili kusogeza huduma hizi bora za afya kwa wananchi ikiwa ni pamoja na kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili".

Kwa upande wake, Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu amesema kuwa hospitali hiyo ni kati ya sita mpya ambazo Serikali imejenga katika mikoa ya Katavi, Songwe, Geita, Mara na Simiyu ili kuboresha huduma za afya na kusogeza huduma za kibingwa karibu na wananchi.

"Hospitali hii ina majengo ya kisasa ya mama na mtoto, wagonjwa wa nje, maabara, huduma za dharura, jengo la kuhifadhia maiti, nyumba 6 za watumishi na wodi yenye uwezo wa kulaza wagonjwa 240". Amesema Waziri Ummy.

Naye, Mganga Mfawidhi wa hospitali hiyo, Daktari Winfred Kyambile amesema kuwa hospitali hiyo itahudumia pia wagonjwa kutoka mikoa ya Ruvuma, Iringa na Mbeya.

Aidha, Mkazi wa Mgodechi, Njombe Bw. Steven Ngailo ameeleza kuwa hospitali hiyo ni mkombozi kwao kwa vile itatatua changamoto za kiafya zilizokuwa zinawakabili.

"Tulikua tunapata huduma mbali na hospitali zetu zilikuwa na uwezo mdogo wa matibabu au tutumie gharama kubwa kwenda Hospitali ya Rufaa Mbeya sasa hata wake zetu watapata huduma za akina mama zenye ubora zaidi tunaishukuru sana Serikali" Amesema Ngailo.

Rais Samia yuko katika ziara ya siku nne mkoani Njombe ambapo atakagua na kuzindua miradi mbalimbali ya maendeleo pamoja na kuzungumza na wananchi.

No comments:

Post a Comment