Na Okuly Julius-Dodoma
MAMLAKA ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA) imetoa wito kwa wafugaji kuacha kununua dawa za mifugo kiholela katika minada na magulio ili kuepuka kuuziwa dawa ambazo hazikidhi vigezo vya ubora, usalama na ufanisi kwani kunahatarisha afya za mifugo yao na afya za walaji.
Hayo yameelezwa na Meneja wa TMDA Kanda ya Kati, Bi. Sonia Mkumbwa wakati akizungumza na Waandishi wa Habari katika banda la Mamlaka hiyo katika maonesho ya nane nane yanayoendelea katika viwanja vya nanenane - Nzuguni Jijini Dodoma.
Aidha, Bi. Mkumbwa amebainisha kuwa TMDA ina jukumu la kuhakikisha kuwa bidhaa za dawa zikiwemo za mifugo, vifaa tiba na vitendanishi vina ubora kwa kuzingatia vigezo vilivyowekwa kimataifa na kitaifa kwa kufanya usajili wa bidhaa hizo, ukaguzi wa viwanda na maeneo ya kutolea bidhaa hizo ili kuendelea kumlinda mwananchi.
“TMDA inahakikisha inafuatilia ubora wa bidhaa hizo mara kwa mara katika soko kwa kufanya kaguzi katika maeneo ya kuzalishia, kutunzia na kuuzia ili kuhakikisha matoleo yaliyopo katika soko yanakidhi vigezo ikiwapo kufanya uchunguzi wa kimaabara. Lakini pia maabara yetu imethibitishwa na Shirika la Afya Duniani (WHO) na endapo mamlaka itabaini kuna bidhaa zisizo na ubora basi hatua za kisheria huchukuliwa kwa waliokiuka ikiwemo uteketezaji wa bidhaa hizo pamoja na tozo za faini kwa mujibu wa Sheria”, Amesema meneja huyo.
Vilevile, amesema TMDA inaendelea kufuatilia usalama wa bidhaa inazodhibiti na inatoa rai kwa wananchi kutoa taarifa endapo watapata madhara yoyote kutokana na matumizi ya bidhaa hizo.
TMDA Kanda ya Kati imeshiriki katika maonesho ya Sikukuu ya wakulima na wafugaji (nanenane) kwa lengo la kuendelea kutoa elimu juu ya matumizi sahihi ya bidhaa inazozidhibiti kwa wananchi hususan wafugaji ili kuendelea kulinda afya ya jamii na kuleta tija katika uchumi wa taifa.
No comments:
Post a Comment