Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara Serikali imesena kuwa inaendelea kuchukua hatua mbali mbali kwa lengo la kuwapunguzia Wananchi athari zitokanazo na kupanda kwa bei za bidhaa muhimu.
Hayo yamesemwa na Waziri wa uwekezaji, viwanda na biashara Dkt. Ashatu K. Kijaji leo August 15,2022 jijini Dodoma wakati akizungumza na waandishi wa habari wakati akiwasilisha tathmini ya mwenendo wa bei ya bidhaa muhimu nchini.
Dkt. Kijaji amesema kuwa lengo la tathmini hiyo ni kumlinda mlaji kwa kuhakikisha anapata bidhaa bora kwa bei stahiki na kuzuia upandishwaji holela wa bei za bidhaa mbalimbali, pamoja na kuchukua hatua za kisheria kwa yeyote atakayebainika kupandisha bei za bidhaa kiholela bila kuzingatia gharama halisi za uzalishaji au uingizaji nchini wa bidhaa husika.
“ Matokeo ya tathmini zilizofanyika hivi karibuni yameonesha kuwa kuna uhimilivu mkubwa wa bei (price stability) kwa bidhaa zinazozalishwa hapa nchini, ambazo zilionesha ongezeko dogo la bei ikilinganishwa na bidhaa zinazoagizwa kutoka nje ya nchi ambazo zilionesha ongezeko kubwa zaidi la bei,”amesema.
Aidha, ameongeza kuwa serikali imepunguza ushuru kwa malori yanayosafirisha bidhaa (transit charges) kutoka Dola za Marekani 16 kwa kila kilomita 100 hadi Dola za Marekani 10 kwa kila kilomita 100 ili kupunguza gharama za usafirishaji wa bidhaa nchini na hivyo kuleta unafuu wa bei za bidhaa hizo.
Amesema serikali pia imeondoa ushuru wa forodha kwa kutoza kiwango cha asilimia sifuri (0%) badala ya asilimia 10 kwenye malighafi za utengenezaji wa sabuni (RBD Palm Stearin) kwa lengo la kuhamasisha na kupunguza gharama za wazalishaji wa ndani wa sabuni ili kudhibiti ongezeko la bei ya sabuni.
“Serikali inatekeleza Mkakati wa kuongeza uzalishaji wa ndani wa mafuta ya kula ikiwa ni pamoja na kuhamasisha wakulima kutumia mbegu bora za alizeti na chikichi (mawese) ili kuongeza uzalishaji wa mafuta ya kupikia yatokanayo na mazao hayo.
“Ongezeko la bei ya mafuta duniani lina athari hasi kwetu Watanzania, kwani mahitaji ya mafuta ndani ya Taifa letu kwa mwaka ni tani 650,000 (MT) huku uwezo wetu wa kuzalisha mafuta ni tani 270,000 (MT), ambayo ni sawa na asilimia 41.5 tu ya mahitaji yetu kwa mwaka,”amesema.


No comments:
Post a Comment