Na Okuly Julius-Dodoma
Mamlaka ya majisafi na usafi wa mazingira jiji la Arusha (AUWSA), imewataka wananchi wa Arusha kuendelea kutunza miundombinu ya maji pamoja na vyanzo vyake ili kurahisisha upatikanaji wa huduma bora za maji.
Hayo yamesemwa leo August 10,2022 Jijini Dodoma na Mkurugenzi mtendaji wa mamlaka hiyo Mhandisi Justine Rujomba wakati akizungumza na waandishi wa habari kwenye kikao cha uwasilishaji wa taarifa ya utekelezaji wa shughuli za mamlaka hiyo na mwelekeo wa utekelezaji kwa mwaka wa fedha 2022/23.
Amesema ikiwa watumiaji hao wa maji watatumia nguvu kutunza vyanzo vya maji na usafi wa Mazingira uzalishaji maji utaongezeka mara dufu na kuendana na mahitaji yaliyopo.
Licha ya hayo amefafanua kuwa kiasi cha maji kwa jiji la Arusha kimeongezeka kwa lita 26,000,000 kwa siku na kwamba ongezeko hilo limewezesha kuboresha wa upatikanaji wa maji kwenye maeneo yaliyokuwa na uhaba wa maji .
Ameyataja maeneo hayo kuwa ni pamoja na Moshono, Kiserian, Murrieti, Olasiti, Sombetini, Kwa Moromboo, Olmoti, Sokoni 1, na baadhi ya maeneo ya Terati na kufafanua kuwa ongezeko hili limechangia kuongeza saa za huduma kutoka masaa 15 hadi 19.
Katika kuboresha zaidi upatikanaji wa huduma hiyo, Rujomba amesema kuwa Serikali kupitia fedha za mkopo wa riba nafuu kutoka Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) imewekeza katika kuboresha hali ya upatikanaji wa huduma ya maji safi na uondoaji wa majitaka katika jiji la arusha.
Amesema hadi kufikia mwezi Julai mwaka huu utekelezaji wa mradi mkubwa umefikia asilimia 90, ambapo kupitia utekelezaji wa mradi huo wananchi wa Arusha wameanza kunufaika na vipengele vya mradi vilivyo kamilika.
“ Hadi mwezi Juni 2022, mradi umewanufaisha wananchi 1,064 kwa kuwalipa fidia kiasi cha Shilingi 5,790,793,407 kwa kutwaa maeneo yao kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya mradi mkubwa,”amesema.
Aidha ameongeza AUWSA imefanikiwa kukamilisha utekelezaji wa miradi ya maji ya Karatu Tom kwa gharama ya Shilingi million 623.4, Ayalabe Karatu (Kwa gharama ya shilingi milioni 714.7), pamoja na mradi wa maji wa maeneo ya pembezoni mwa Jiji la Arusha unaofadhiliwa na fedha za UVIKO 19 (kwa gharama ya shilingi milioni 575) huku miradi yote hiyo ikihudumia wananchi wote kama ilivyokusudiwa.
Mamlaka ya majisafi na usafi wa mazingira jiji la Arusha (AUWSA) ni taasisi ya Serikali inayofanya kazi zake chini ya Wizara ya Maji ambapo mamlaka hiyo ilianza kufanya kazi zake Julai 1, 1998 baada ya kuanzishwa kwa sheria ya maji ya mwaka 1997 iliyobadilishwa na Sheria ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Na. 5 ya Mwaka 2019 ikiwa na majukumu ya kuhakikisha inatoa huduma bora za majisafi na uondoaji wa majitaka kwa ufanisi na kwa uhakika kwa kutumia rasilimali na teknolojia iliyopo kwa maendeleo endelevu ya Jiji la Arusha na Tanzania kwa ujumla.

No comments:
Post a Comment