Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dkt Dorothy Gwajima amesisitiza wazazi na walezi kutimiza majukumu yao ipasavyo kwa mujibu wa sheria, tamaduni na mila za kiafrika za kuhakikisha watoto wanatimiziwa mahitaji yao ya msingi, kuendelezwa katika fursa mbalimbali pamoja na kulindwa ili familia iwe mahali salama kwa watoto kulelewa na kufurahia haki zao.
Kufanya hivyo itapunguza idadi ya Watoto wanaoishi mazingira hatarishi na kupelekea hitaji la kulelewa makaoni.
Mh. Gwajima ameyasema hayo leo Agosti 17,2022 katika maadhimisho ya Miaka 20 tangu kuanzishwa kwa Makao ya Kijiji cha Matumaini Jijini Dodoma ,huku akitoa wito kwa wadau wote ikijumuisha vyombo vya habari, watoa huduma za ustawi wa familia na viongozi wa dini kuungana kutoa elimu kwa jamii, wazazi na walezi kuhusu umuhimu wa kuimarisha stadi za malezi na kuwatunza watoto kuanzia ili kuwaepusha na hatari na changamoto zinazozuilika na kuepuka kuongeza idadi ya watoto wanaoishi katika mazingira hatarishi.
Aidha, Dkt.Gwajima amesema kwa serikali imeweka utaratibu wa kuhakikisha watoto wanaokosa malezi wanapatiwa malezi mbadala kupitia huduma ya Makao ya Watoto, watu wa kuaminika, malezi ya kambo na kuasiliwa huku huduma hizo zikiratibiwa na kamishna wa Ustawi wa Jamii kupitia Maafisa Ustawi wa Jamii waliopo katika Halmashauri zote Nchini.
Dkt. Gwajima amesema kuwa Idadi ya watoto wanaolelewa katika Kijiji cha Matumaini ni 145 (wakiume 62, wakike 83) ikiwa ni sehemu ya watoto takribani 24,254 (wakiume 10,923, wakike13,331) wanaolelewa katika Makao ya Watoto 324 yaliyosajiliwa hapa nchini ambapo makao 322 ni ya binafsi na mawili (2) ni ya Serikali yaliyopo Kurasini, Manispaa ya Temeke Dar es Salaam na Kikombo Jijini Dodoma.
"Ndugu Waalikwa, Idadi ya watoto wanaolelewa katika Kijiji cha Matumaini imeelezwa kuwa ni 145 (Me 62, Ke 83). Hii ni sehemu ya watoto takribani 24,254 (Me 10,923, Ke 13,331) wanaolelewa katika Makao ya Watoto 324 yaliyosajiliwa hapa nchini ambapo makao 322 ni ya binafsi na mawili (2) ni ya Serikali yaliyopo Kurasini, Manispaa ya Temeke Dar es Salaam na Kikombo Jijini Dodoma".Amesema Gwajima.
Kwa Upande, Askofu Mkuu wa Jimbo Katoliki Dodoma Beatus Kinyaiya amewataka watoto wanaoishi katika kijiji cha Matumaini wafuate kila kitu kizuri wanachofundishwa na walimu ili kuwa zao zuri katika taifa kwa ujumla.
Pia,ameiomba serikali kukifanya kituo hicho kuwa cha hisani ili kufanya michango yote inayopatikana kutumika katika kulea watoto wanaoshi katika kijiji cha matumaini na Mamlaka ya mapato tanzania iache kuchukua kodi.
"Tunaomba utufikishie ombi letu kwa serikali itusaidie kubadilisha kituo hichi kuwa cha hisani ( Kisilipe kodi) kiondolewe kodi kabisa ili kile kinachopatikana kilenge kutoa msaada kwa watoto waliopo katika kituo hiki kwa sababu kile kile kidogo kinachopatikana tukigawana tena na TRA sasa itakuaje hivyo tunaomba hili liangaliwe kwa kweli ,"Amesema Askofu Kinyaiya
Hata hivyo, huduma ya malezi katika Makao ya Watoto ni suluhisho la mwisho na la muda mfupi kwa mtoto wakati changamoto zilizopelekea kupelekwa makaoni zikifanyiwa kazi ili mtoto arejeshwe katika familia yake au kutafutiwa malezi ya kifamilia kupitia Malezi ya Kambo au Kuasili.







No comments:
Post a Comment