AWESO ABEBA AGENDA YA MAJI KATIKA MKUTANO WA 13 WA KAMATI TENDAJI YA BARAZA LA MAWAZIRI WA MAJI WA AFRIKA - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Thursday, October 13, 2022

AWESO ABEBA AGENDA YA MAJI KATIKA MKUTANO WA 13 WA KAMATI TENDAJI YA BARAZA LA MAWAZIRI WA MAJI WA AFRIKA


Na Mwandishi wetu - Windhoek, Namibia

Waziri wa Maji, Mheshimiwa Jumaa Hamidu Aweso (Mb) ameiwakilisha Tanzania katika Mkutano wa 13 wa Kamati Tendaji (Executive Council-EXCO) ya Baraza la Mawaziri wa Maji wa Afrika (African Ministers’ Council on Water – AMCOW) umefanyika tarehe 13 Oktoba 2022, Jijini Windhoek nchini Namibia.

Katika Mkutano huo, AMCOW ambayo ni Taasisi ya Umoja wa Afrika wamejadili masuala mbalimbali kuhusu Dira ya Maji ya Afrika ya mwaka 2025; agenda ya maji Barani Afrika ikiwa ni pamoja na kuimarisha uwekezaji katika Sekta ya Maji ambayo ni kiungo cha kufikia malengo Endelevu ya Umoja wa Mataifa 2015-2030 na Agenda ya Afrika ya Mwaka 2063.

Vilevile, mkutano umeandaa ujumbe wa Sekta ya Maji Afrika katika Mkutano wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi utakaofanyika mwezi Novemba 2027 nchini Misri maarufu kama COP27; na kukubaliana kuwasilisha Azimio la Dakar kuhusu maji katika Mkutano wa Umoja wa Mataifa kuhusu maji utakaofanyika Marekani mwaka 2023 (The UN Water 2023 conference). 

Aidha, Mheshimiwa Aweso amehimiza umuhimu wa Afrika kuipa hadhi na agenda ya maji kupitia kuimarisha uwekezaji katika Sekta ya Maji kwa kuwa maji ni kiungo cha maendeleo kupitia usalama wa chakula, usalama wa nishati, afya ya jamii, mazingira, uhimilivu wa mabadiliko ya tabianchi, misitu na viwanda miongoni mwa masuala mengine. 

Katika hatua nyingine, Mheshimiwa aweso amesisitiza kuwa Tanzania itaendelea kushirikiana na AMCOW katika kuboresha usimamizi wa rasilimali za maji, usambazaji maji na usafi wa mazingira nchini.

No comments:

Post a Comment