Na Mwandishi wetu Singida
Mkuu wa mkoa wa Singida Mhe. Peter J. Serukamba leo tarehe 13 Oktoba 2022 ameshudia utiaji saini wa mkataba wa ujenzi wa mradi wa majitaka kati ya Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Singida (SUWASA) na mkandarasi (M/S Perntels Company and Nangai Engineering and Contractors Co.(T) LTD (JV ) iliyofanyika ukumbi wa Bonde la Kati.
Katika hafla hiyo iliyo hudhuriwa na viongozi mbalimbali wa chama na Serikali, Mhe. Serukamba ameishukuru Serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora.
Mhe. Serukamba ameipongeza SUWASA kwa kubuni na hatimaye kuanza utekelezaji wa mradi huo kwa maendeleo ya mkoa wa Singida.
Vilevile ameitaka SUWASA ihakikishe inamsimamia vyema mkandarasi ili kazi ikamilike kwa wakati kwani Serikali imewekeza fedha nyingi katika mradi huu pia ameshauri SUWASA kuangalia uwezekano wa kutumia teknolojia mpya ya kutibu maji ili yaweze kuwa na ubora wa kutosha kuweza kutumiwa na binadamu, jambo litakalosaidia kuondoa upungufu wa maji katika Manispaa ya Singida.
Mhe. Serukamba ametoa pongezi kwa uongozi wa Manispaa ya Singida hususani Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa ya Singida, Ndugu Jeshi Lupembe kwa ushirikiano mkubwa ambao wameipatia SUWASA katika hatua mbalimbali za upatikanaji wa eneo la ujenzi wa mradi huo.
Mwenyekiti wa Bodi ya SUWASA Deocres Kamala ameishukuru Serikali kwa kutoa kiasi cha shilingi bilioni 1.7 ili kugharamia ujenzi wa mabwawa matatu ya kutibu majitaka na ununuzi wa gari moja la kunyonya majitaka kutoka kwenye makazi ya watu.
Aidha Mkurugenzi wa SUWASA ndugu Sebastian Warioba pia ameishukuru Serikali kwa kuridhia utekelezaji wa mradi huu ambapo amesema mradi huu utakapokamilika utawanufaisha wananchi wapatao 259,539 hadi ifikapo mwaka 2036 kwa kuongeza tija katika kilimo cha umwagiliaji, utaongeza ajira na kuboresha usafi wa mazingira katika Manispaa ya Singida
No comments:
Post a Comment