Na. Getruda Shomi, DODOMA
MKUU wa Wilaya ya Dodoma, Jabir Shekimweri asisitiza wazazi kuwajengea watoto wao uwezo wa kujiamini na kujieleza ili iwe rahisi kutoa taarifa pale inapotokea wanafanyiwa vitendo vya ukatili wa kijinsia.
Ameyasema hayo katika ufungaji wa mashindano ya midahalo baina ya shule za sekondari zilizopo katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma, yaliyofanyika katika ukumbi wa shule ya sekondari Dodoma.
Shekimweri ameeleza kuwa watoto hushindwa kutoa taarifa za ukatili wa kijinsia kwasababu hawawezi kujieleza pale wanapofanyiwa ukatili. “Kama watoto wetu tukawafundisha na kuwajengea kujiamini na kujenga hoja ni ngumu mtu mwenye dhamira mbaya kufanya vitendo vya ukatili wa kijinsia”. Amesema Shekimweri.
Ameongeza kuwa tafiti zinaonesha miongoni mwa wanaosababisha ukatili wa kijinsia ni ndugu wa karibu wa familia.“ Unakuta mjomba, bamkubwa ndio wanaofanya ukatili kwa watoto, hivyo watoto wakiwa na kujiamini wataweza ‘kuraise voice’ kwamba vitu hivyo havifai”
Aidha, Mwanafunzi wa Shule ya Sekondari Mnadani Haruna Jumaa ametoa ushauri kwa wanafunzi wenzake kuchukua hatua wanapofanyiwa vitendo vya ukatili alisema kuwa, ukatili hauwezi kuwa ukatili kama muathirika hataweza kutoa taarifa na hiyo hutokana na kutokujiamini.
“Ukiona kitendo kinataka kutokea au kimekwisha kutokea toa taarifa kwa vyombo husika au hata kwa waliokuzidi umri ili waweze kupata namna ya kukusaidia”. Amesema Haruna.
Naye Mratibu wa Mashindano ya Mdahalo, Mwalimu Marick Masoud ametoa ufafanuzi wa mada zilizofanyiwa mdahalo mojawapo ikiwa ni kupinga ukatili wa kijinsia alieleza kuwa, lengo ni kuona namna gani wanafunzi wanashindwa kufikia malengo yao kutokana na ukatili wa kijinsia na namna ukatili huo unavyowaathiri.
“Watoto wanashindwa kufikia malengo yao kutokana na mambo ya ukatili wa kijinsia. Alisema Marick.
Mashindano hayo ya mdahalo yaliyoanza tangu Octoba 1, 2022. yakijumuisha shule 16 zilizopo ndani ya Jiji la Dodoma yalifikia ukomo jana Jumatatu na Miyuji Sekondari waliibuka mshindi wa jumla.



No comments:
Post a Comment