Na Okuly Julius-Dodoma
Kufuatia uchambuzi uliofanyika baada ya kuondolewa kwenye Utumishi wa Umma watumishi hao wamekuwa wakitumia njia mbalimbali, ikiwa ni pamoja na kutumia Vyama vya Wafanyakazi kuomba walipwe mafao kutoka kwenye mifuko hiyo.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Oktoba 27,2022 jijini Dodoma Waziri wa Nchi,Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi,Vijana,Ajira, na Wenye Ulemavu) Prof.Joyce Ndalichako kufuatia maelekezo hayo ,amesema kuwa Mifuko ya Hifadhi ya jamii ya PSSSF na NSSF itarejesha michango ya Wafanyakazi iliyowasilishwa kwenye Mifuko hiyo bila kuhusisha michango ya mwajiri.
"Kama mnavyokumbuka katika kipindi cha kuanzia Mwezi Oktoba, 2016 hadi April,2017 ,Serikali iliendesha zoezi maalum la uhakiki wa vyeti kwa kushirikiana na Baraza la Mitihani la Taifa ( NACTE),kufuatia Uhakiki huo ,watumishi wasiopungua 14,516 walibainika kuwa na vyeti vya kughushi na walioondolewa katika utumishi wa Umma,"
Na kuongeza kuwa "Wakati wa maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani tarehe 01 Mei ,2022 ,Shirikisho la Vyama Vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA) kupitia risala yao,waliwasilisha ombi kwa Mheshimiwa Rais aangalie namna ya kuwafuta Jasho lao ambapo Rais katika hotuba yake kwenye siku hiyo alielekeza kufanyika kwa uchambuzi ili kuona namna gani ambavyo Serikali inaweza kuhitimisha suala hilo,"amesma Prof.Ndalichako
Aidha, Prof.Ndalichako amewataka waajiri kuwajibika kuwasilisha kwenye Mifuko Hati za Ridhaa pamoja na nyaraka nyingine zinazohusu ulipaji wa mafao kwa kuzingatia taratibu na miongozo ya Mifuko husika.
"Mara baada ya Mifuko Kupokea nyaraka kutoka kwa aliyekuwa Mwajiri,malipo yatafanyika kupitia akauti za benki na marejesho ya michango ya Watumishi hao, yataanza kufanyika kuanzia tarehe 1 Novemba, 2022,"ameeleza Prof.Ndalichako
Kwa upande wake Waziri wa nchi ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe.Jenista Mhagama amesema kuwa hatua hii iliyochukuliwa na Mhe.Rais ni ya huruma na upendo mkubwa kwa Watumishi hao.
Hivyo Mhagama akawataka Waajiri wote nchini kutoa ushirikiano kwa Watumishi wakati wa kutekeleza zoezi hilo na kujiepusha na vitendo vya rushwa ambavyo vinaweza kuchelewesha na kupelekea kuharibu dhamira njema ya Mhe.Rais.
"Niwaagize Waajiri wote kutekeleza zoezi hili kwa kuzingatia misingi ya utawala bora ikiwemo kuepukana na vitendo vyovyote vitakavyoashiria uwepo wa Rushwa katika kutimiza adhma hii ya Serikali,"Mh.Mhagama
Mhe.Mhagama ametoa wito kwa TAKUKURU kutumia kila mbinu kuhakikisha wanazuia vitendo vyote vya Rushwa pindi zitakapojitokeza.
No comments:
Post a Comment