Na Gideon Gregory-Dodoma
MKURUGENZI Mkuu wa Mfuko wa hifadhi ya jamii (PSSSF),CPA Hosea Kashimba amesema kuwa wanatarajia kuhakikisha mifumo ya PSSSF inasomana na mifumo mingine kutoka Taasisi za Umma zinazotoa huduma ili kurahisisha uandikishaji wa wanachama na uletaji wa madai kupitia mtandao na kutumia mifumo mipya ya Tehama kulingana na mahitaji ya Mfuko.
Matarajio mengine ni kubuni mifumo mipya na salama ya TEHAMA kulingana na mahitaji ya mfuko pamoja na kutumia mifumo ya TEHAMA kwa asilimia 85 huku lengo likiwa ni kutumia kwa asilimia 100 ifikapo 2023 katika shughuli za Mfuko hivyo kuboresha utoaji huduma.
CPA Hosea ameyasema hayo leo Novemba 09,2022 Jijinin Dodoma wakati akizungumza na Waandishi wa habari kuhusu Utekelezaji wa Shughuli mbalimbali za Mfuko huo huo na utekelezaji wake kwa mwaka wa fedha wa 2022-2023.
" Matarajio yetu menginenya baadae ni kuongeza vituo vya uhakiki Katika halmashauri mbalimbali na kuanzisha utaratibu wa kujihakiki kupitia simu janja na kusaidia Kila taarifa ya mwanachama iwe kwenye mfumo,"Amesema CPA Hosea
CPA Hosea ameongeza kuwa ili jitihada za kuhakikisha lengo la kutoa huduma bora linatimia,Mfuko unaendelea kutekeleza mambo mbalimbali yanayolenga kurahisisha utoaji wa huduma ikiwa ni pamoja na mtandao wa Ofisi za Mfuko ambapo una Ofisi Kila Mkoa na baadhi ya Wilaya Kwa lengo la kuwa karibu na wanachama.
“Mfuko una kituo cha kupiga simu bure kwa ajiri ya wanachama ambapo huduma hutolewa hadi saa mbili usiku ikiwemo mfumo wa ufuatiliaji wa masuala ya yanayohusu huduma mbalimbali za uanachama,”amesema CPA Kashimba.
Pia,Murugenzi huyo amesema kuwa mfuko huo unatarajia kutumia kiasi cha shilingi Bilioni 20 kuwalipa watumishi wa Umma 9000 waliondolewa kazini kwa sababu ya vyeti feki.
Hatua hiyo imekuja kufuatia agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan kutaka watumishi hao walipwe michango yao waliyochangia kwenye mifuko ya hifadhi ya jamii ambapo aliagiza utekelezaji huo uanze Novemba Mosi,2022.
“Ili walengwa hao wapate stahiki zao wanapaswa kufuata taratibu za uajiri ambapo wanatakiwa kuwasilisha madai yao Kwa waajiri ili kupeleka vielelezo kwenye Mfuko huo kisha marejesho ya michango Yao kuanza kufanyika kuanzia tarehe moja, Novemba, na kusisitiza kuwa wangependa jambo hilo likamilike ndani ya muda mfupi,”amesema CPA Hosea.
Amefafanua kuwa ili kuwezesha malipo hayo kufanyika mtumishi husika atatakiwa kwenda kwa aliyekuwa mwajiri na kuchukua nyaraka zote muhimu ambazo zinatakiwa na PSSSF ndipo atapata malipo yake.
CPA Hosea Kashimba amesema gharama za uendeshaji wa mfuko huo zimepungua kwa mwaka kutoka Shilingi bilioni 128.93 mwaka 2018 hadi shilingi bilioni 68.83 sawa na kushuka kwa asilimia 46.61 kutokana na uunganishwaji wa mifuko minne.
Ambapo amesema uunganishwaji wa mifuko hiyo minne imeleta uendelevu wa mifuko kwani umenusuru udororaji wa mifuko na kuanzishwa kwa mfuko wa PSSSF ambao umeongeza ufanisi wa utoaji huduma.
Amesema kuwa uunganishwaji huo umeondoa ushindani usio na tija kwani kumekuwepo na mifuko ya pensheni miwili yenye majukumu tofauti ya mmoja kuhudumia sekta binafsi na mwingine sekta ya umma.
“Uunganishwaji huu umewezesha kuwianisha mafao yatolewayo na mifuko ya pensheni ambapo kuanzia Julai 1,mwaka huu wanachama wote wa mifuko ya pensheni wanalipwa mafao ya uzee kwa kutumia kanuni zinazofanana ambazo zinalipa mafao bora na kuwezesha mifuko,”amesema CPA Hosea.
Pamoja na hayo CPA Kashimba ameeleza kuwa Mfuko huo unatambua Moja ya changamoto kubwa kwenye jamii ni uelewa mdogo kuhusu sekta ya hifadhi ya jamii hivyo PSSSF imejipanga kuendelea kutoa elimu kwa wanachama wake ili kuhakikisha sekta hiyo inafanikiwa .
Amesema kuwa ili jitihada za kuhakikisha lengo la kutoa huduma bora linatimia,Mfuko unaendelea kutekeleza mambo mbalimbali yanayolenga kurahisisha utoaji wa huduma ikiwa ni pamoja na mtandao wa Ofisi za Mfuko ambapo una Ofisi Kila Mkoa na baadhi ya Wilaya Kwa lengo la kuwa karibu na wanachama.
“Mfuko una kituo cha kupiga simu bure kwa ajiri ya wanachama ambapo huduma hutolewa hadi saa mbili usiku ikiwemo mfumo wa ufuatiliaji wa masuala ya yanayohusu huduma mbalimbali za uanachama,”amesema CPA Kashimba.
Ikumbukwe kuwa mfuko wa PSSSF ulianzishwa mwaka 2018 kupitia sheria ya mfuko wa hifadhi ya jamii kwa watumishi wa Umma Namba 2 ya mwaka 2018 ambapo mfuko huo ni matokeo ya kuunganishwa kwa iliyokuwa mifuko ya hifadhi ya jamii ya GEPF (1942),LAPF (1944),PPF (1978) na PSPF(1999).
No comments:
Post a Comment