Katika kuhakikisha msingi wa Sera ya Afya ya mwaka 2007 kwamba "KINGA NI BORA KULIKO TIBA" inazingatiwa, Wizara Ya Afya imeamua kubeba jukumu la kusimamia Usafi wa Mazingira moja kwa moja kupitia Idara ya Kinga ili kuepukana na magonjwa ya mlipuko.
Akizungumza leo Novemba 19,2022 Jijini Dodoma, wakati wa kilele cha Wiki ya Usafi wa Mazingira Kitaifa na Siku ya Matumizi wa Choo Duniani na utoaji wa tuzo za Usafi,Naibu katibu Mkuu Wizara ya Afya Dkt.Seif Shekalaghe amesema kuwa ,usafi wa mazingira kwa ujumla wake unachangia kwa sehemu kubwa kuzuia magonjwa ya kuambukiza na yasiyoambukiza.
"Kwa kuwa leo ni kilele cha Wiki ya Usafi wa Mazingira nchini, napenda kuikumbusha jamii umuhimu wa kuweka mazingira katika hali ya usafi,Sote ni mashahidi kwamba, hali ya usafi katika maeneo mengi bado si ya kuridhisha sana,atika baadhi ya maeneo udhibiti wa taka ngumu na majitaka haufanyiki kwa kiwango cha kuridhisha na hivyo kupelekea kuwepo kwa uchafu uliokisiri hali inayohatarisha afya ya jamii,
Na kuongeza kuwa " Kutokana na msingi huu, Serikali kupitia Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa imeunda Kitengo katika Halmashauri zote kusimamia suala la Udhibiti wa Taka na Usafi. Kitengo hiki kina jukumu la kusimamia shughuli zote za usafi wa mazingira katika Halmashauri. Wizara ya Afya kupitia vitengo hivi imebeba jukumu la kutoa Miongozo ya Kisera kwenye Kitengo hiki ili kiweze kutekeleza vema majukumu yake kwani madhara ya uchafu huigusa sekta ya afya zaidi pengine kuliko sekta nyingine yoyote,Mfano, kunapotokea magonjwa ya mlipuko kama vile, kipindupindu, kuhara, kuhara damu; sekta ya afya ndio hubeba jukumu kwa sehemu kubwa kukabiliana na milipuko ya aina hii,"Amesema Dkt.Shekalaghe
Dkt.Shekalaghe amedokeza kuwa ,uwepo wa vyoo bora kwa upande wa kaya umeongezeka sana katika kipindi cha miaka kumi iliyopita ambapo kwa sasa vyoo bora katika ngazi ya kaya umeongezeka kutoka asilimia 19.5 mwaka 2012 hadi kufikia asilimia 72.6 mwaka 2022,huku Kaya zisizokuwa na vyoo kabisa zimepungua kutoka asilimia 20.5 hadi kufikia asilimia 1.4 sasa.
Aidha,Dkt.Shekalaghe amesema khwa ujenzi wa vyoo bora pamoja na uwepo wa huduma za maji safi na salama umeongezeka katika taasisi mbalimbali ikiwemo shule za msingi na vituo vya kutolea huduma za afya,ambapo ndani ya kipindi cha miaka mitatu iliyopita takriban shule za msingi 2,500 zimejengewa vyoo bora, huku vituo vya kutolea huduma za Afya vipatavyo 1,500 vimeboreshewa huduma ya maji, vyoo na sehemu za kunawa mikono.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi Msaidizi wa Afya Mazingira Anyikite Mwakitalima,amesema kuwa dhima ya Wizara ya kuhakikisha afya bora kwa kila mwananchi inatimia, hakuna chaguo jingine zaidi ya kuwekeza nguvu na rasilimali za kutosha kwenye eneo la Kinga hususani Afya Mazingira.
" Ripoti ya Benki ya Dunia inaeleza kwamba tunapowekeza shilingi moja kwenye usafi wa mazingira tunaokoa shilingi tisa (9) ambazo zingetumika kwa namna yeyote kugharamia madhara ambayo yangetokana na uchafu ikiwemo gharama za kutibu magonjwa, muda wa uzalishaji unaopotea, vifo vya mapema na athari nyingine nyingi,
Na kuongeza kuwa "Kwa kulitambua hili, Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeongeza uwekezaji kwenye eneo la usafi wa mazingira. Serikali imetenga zaidi ya shilingi bilioni 104 kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya Usafi na huduma za maji kwenye shule za msingi na vituo vya huduma za afya. Kiasi hiki kinatumika kwenye shule za msingi 1500 na zaidi ya vituo vya huduma za afya 2500,"Amesema Anyikite Mwakitalima
Aidha, Anyikite Mwakitalima amesema kuwa Serikali imeandaa fedha kupitia mradi wa BOOST chini ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia ambao utawezesha ujenzi wa miundombinu bora ya usafi kwa shule zaidi ya 6000 ifikapo mwaka 2025.
Katika kuimarisha Usafi, Wizara ya Afya imekuwa ikisimamia uendeshaji wa Mashindano ya Afya na Usafi wa Mazingira kwa lengo la kudumisha tabia ya kupenda Usafi kote nchini.
Mashindano haya huanza katika ngazi ya Kitongoji na kisha Kijiji, Mtaa, Kata, Halmashauri, Mkoa na hatimaye Taifa. Katika mwaka 2022 Mashindano haya yalihusisha Makundi 11 ambapo matokeo yake ni kama ifuatavyo;
Kundi la Kwanza Halmashauri za Majiji
Mshindi wa Tatu: Halmashauri ya Jiji la Tanga (80%)
Mshindi wa Pili: Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam (81%)
Mshindi wa Kwanza: Halmashauri ya Jiji la Arusha (85%)
Nafasi ya mwisho katika kundi hili imeshikwa na Halmashauri ya Jiji la Mbeya ambalo limepata asilimia 56.
Kundi la Pili Halmashauri za Manispaa
Mshindi wa Tatu: Halmashauri ya Manispaa ya Moshi (82%)
Mshindi wa Pili: Halmashauri ya Manispaa ya Iringa (85%)
Mshindi wa Kwanza: Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga (87%)
Nafasi ya mwisho katika kundi hili imeshikwa na Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro iliyopata 44%.
Kundi la Tatu Halmashauri za Miji
Mshindi wa Tatu: Halmashauri ya Mji wa Njombe (72%)
Mshindi wa Pili: Halmashauri ya Mji wa Mafinga (75%)
Mshindi wa Kwanza: Halmashauri ya Mji wa Babati (77%)
Nafasi ya mwisho imeshikwa na Halmashauri ya Mji wa Ifakara iliyopata 25%
Kundi la Nne Halmashauri za Wilaya
Mshindi wa Tatu: Halmashauri ya Wilaya ya Mji wa Makete (90.6%)
Mshindi wa Pili: Halmashauri ya Wilaya ya Iringa (92.3%)
Mshindi wa Kwanza: Halmashauri ya Wilaya ya Njombe (97.8%)
Nafasi ya mwisho imeshikwa na Halmashauri ya Wilaya ya Itigi iliyopata 35.3%
Kundi la Tano Halmashauri za Vijiji
Mshindi wa Tatu: Halmashauri ya Kijiji cha Lugodalutali, Kata ya Kasanga Halmashauri ya Wilaya ya Mufindi-Iringa (95%)
Mshindi wa Pili: Halmashauri ya Kijiji cha Ibiki, Kata ya Igongolo Halmashauri ya Wilaya ya Njombe-Njombe (97%)
Mshindi wa Kwanza: Halmashauri ya Kijiji cha Image, Kata ya Kidegembye Halmashauri ya Wilaya ya Njombe-Njombe (98%)
Nafasi ya mwisho imeshikwa na Halmashauri ya Kijiji cha Kiwege, Kata ya Ngelengele, Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro, Mkoa wa Morogoro kwa kupata 27%.
Kundi la Sita Halmashauri la Shule za Msingi za Vijijini
Mshindi wa Tatu: Shule ya Msingi Image, Kijiji cha Image,
Kata ya Kidegembye, Halmshauri ya Wilaya ya Njombe (91.2%)
Mshindi wa Pili: Shule ya Msingi Bunazi, Kata ya Kasambi, Halmashauri ya Wilaya ya Missenyi-Kagera (93%)
Mshindi wa Kwanza: Shule ya Msingi Kimashuku, Kata ya Kimashuku, Halmshauri ya Wilaya ya Hai-Kilimanjaro (96.5%)
Nafasi ya mwisho imeshikwa na Shule ya Msingi Njage, Kata ya Mchome, Halmashauri ya Wilaya ya Mlimba-Morogoro kwa kupata 17.5%
Kundi la Saba Shule za Sekondari za Bweni
Mshindi wa Tatu: St. Monica Moshono Girls Secondary School kutoka Jiji la Arusha (96%),
Mshindi wa Pili: Maria De Mathias Secondary School kutoka Jiji la Dodoma (97%),
Mshindi wa Kwanza: Nyankumbu Girls Secondary School kutoka Mji wa Geita (98%)
Nafasi ya mwisho imeshikwa na Sumbawanga Secondary School kutoka Manispaa ya Sumbawanga-Rukwa kwa kupata 36%
Kundi la Nane Hospitali za Rufaa za Mikoa Serikali na Binafsi
Mshindi wa Tatu: Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Temeke (92.8%)
Mshindi wa Pili: Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tanga (Bombo) (93.7%)
Mshindi wa Kwanza: Arusha Lutheran Medical Center (95.5%)
Nafasi ya mwisho imeshikwa na Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Pwani (Tumbi) kwa kupata 54.1%
Kundi la Tisa Hospitali za Wilaya
Mshindi wa Tatu: Hospitali Rubya, Muleba-Kagera (89.2%)
Mshindi wa Pili: Hospitali ya Manispaa ya Kahama-Shinyanga (90.1%)
Mshindi wa Kwanza: Hospitali ya Mugana, Missenyi-Kagera (91.9%)
Nafasi ya mwisho imeshikwa na Hospitali ya Wilaya ya Busokelo, Mbeya (29.7%)
Kundi la Kumi Vyuo Vikuu
Mshindi wa Tatu: University of Dar es Salaam (84.5%)
Mshindi wa Pili: Catholic University of Health and Allied Science (BUGANDO) (89.6%)
Mshindi wa Kwanza: The Nelson Mandela African Institute of Science and Technology (91.2%)
Nafasi ya mwisho imeshikwa na Muslim University of Morogoro kwa kupata 26.9%
Kundi la Kumi na Moja Mabenki
Mshindi wa Tatu: CRDB-Rock City, Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela (94)
Mshindi wa Pili: NBC Cooperate Branch, Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam (96%)
Mshindi wa Kwanza: NBC-Dodoma, Halmashauri ya Jiji la Dodoma (98%).
Nafasi ya mwisho imeshikwa na CRDB Mwanjelwa, Halmashauri ya Jiji la Mbeya kwa kupata 41%.
Kutokana na matokeo hayo, Mkoa uliofanya vizuri zaidi ni Arusha ambaye ndiye mshindi wa jumla na Mkoa uliofanya vibaya zaidi ni Morogoro.
No comments:
Post a Comment