KUNDI LA 17 LENYE WANANCHI 179 LAHAMA KATIKA HIFADHI YA NGORONGORO . - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Thursday, January 12, 2023

KUNDI LA 17 LENYE WANANCHI 179 LAHAMA KATIKA HIFADHI YA NGORONGORO .



Na Kassim Nyaki, NCAA
 
Kundi la 17 la wananchi wanaohama kwa hiari kutoka eneo la Hifadhi ya Ngorongoro kwenda Kijiji cha Msomera na maeneo mengine limeondoka leo tarehe 12 Januari, 2023 baada ya kuagwa na Viongozi wa Mkoa wa Arusha. 
 
Kwa mujibu wa Naibu Kamishna wa Uhifadhi NCAA, Dkt. Christopher Timbuka, kundi linalohama katika awamu hii linajumuisha kaya 34 zenye wananchi 179 pamoja na Mifugo 625.

Ameongeza kuwa kati ya Kaya 34 zinazohama katika awamu hii, kaya 30 zinahamia Kijiji cha Msomera Mkoani Tanga na kaya 4 zinahamia maeneo mengine ya nchi waliyochagua kwa hiari yao.
 
Naibu Kamishna Dkt. Timbuka ameeleza kuwa zoezi la kuhamisha wananchi wa Tarafa ya Ngorongoro waliojiandikisha kuhama kwa hiari kwenda Kijiji cha Msomera lililoanza mwenzi Juni, 2022, hadi kufikia tarehe 12 Januari, 2023 Jumla ya kaya 523 zenye watu 2,808 na mifugo 14,757 zimeshahamia Kijiji cha Msomera na maeneo mengine kwa ajili ya kupisha shughuli za Uhifadhi katika eneo la Ngorongoro.


Akiwaaga wananchi hao Mkuu wa Wilaya ya Ngorongoro Mhe. Raymond Mangwalla amesema zoezi la kuwaandikisha wananchi wanaotaka kuhama kwa hiari ndani ya hifadhi hiyo inaendelea na Serikali inawapa stahiki zao ikiwa ni pamoja na kuwapa fidia inayostahili pamoja na kuwasafirishia mizigo na mali zao kuelekea kwenye makazi mapya.

“Serikali inayoongozwa na Mhe Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imewapa wananchi uhuru wa kuhama kwa hiari, kila mwananchi aliyeko tayari kuhama anafanyiwa tathmini ya mali zake na kupewa fidia pamoja na kuwezeshwa usafiri yeye na mali zake ikiwemo mifugo kwenda eneo alipochagua” ameongeza Mhe Mangwala.

Mhe. Mangwala ameongeza kuwa kadri wananchi wanavyoondoka katika eneo la Hifadhi ya Ngorongoro imeongeza utulivu wa hifadhi na Wanyama hali iliyoongeza hamasa ya utalii hasa kipindi cha mwisho wa mwaka 2022 na mwanzo wa mwaka 2023 ambapo kwa mwezi Desemba, 2022 pekee watalii takribani 63,248 wametembelea vivutio vilivyoko eneo la hifadhi ya Ngorongoro.

Katibu Tawala Mkoa wa Arusha Bw. Masaile Mussa amewaeleza wananchi wa Ngorongoro kuwa Serikali ya mkoa huo itaendelea kuwahakikishia usalama wananchi wote wanaojiandikisha kuhama kwa hiari na misingi yote ya utu na haki za binadamu itazingatiwa.

Bw. Lapajara Tauwo ambaye ni miongoni mwa wananchi wanaohama ameeleza kuwa

 “Mwanzo nilikuwa nasita kuhama lakini baada ya kuwasiliana na wenzangu waliohamia Kijiji cha Msomera nimeona na mimi niondoke nikawe huru kufanya shughuli za uzalishaji mali na ujasiriamali, naamini hata ndugu zetu tuliowaacha Ngorongoro watahamasika na kujiandikisha kwa wingi zaidi ili tuache hifadhi yetu ilete faida kwa maslahi ya watanzania wote”

No comments:

Post a Comment