LAIGWANANI MSOMERA WATOA KONGOLE KWA SERIKALI - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Thursday, February 2, 2023

LAIGWANANI MSOMERA WATOA KONGOLE KWA SERIKALI


Na WMJJWM, Msomera Handeni Tanga.

Wazee wa Mila wa Jamii ya Kimasai, Laigwanani wameipongeza Serikali kwa hatua ya kuwahamishia katika eneo la Msomera lilipo wilayani Handeni, Mkoa wa Tanga wakitokea Ngorongoro.

Wamesema hatua hiyo imewawezesha kufanya shughuli zingine za kijamii ikiwepo kilimo badala ya kutegemea mifugo pekee kama chanzo cha mapato ya familia.

Wazee hao wametoa kauli hiyo mbele ya Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Wakili Amoni Mpanju wakati wa ziara ya Uongozi wa Wizara hiyo kijijini Msomera iliyoanza Februari 01,2023.


Akizungumza kwa niaba ya Malagwanani wenzake Laigwanani Saiyanga Karani alisema kitu kikubwa kilichokuwa kinawasumbua ni uoga wa kutokujua waendako, lakini walipobaini kuwa Serikali ilikuwa na mipango mizuri waliamua kuchukua hatua yakujiandikisha waweze kuhama.

“Mwanzoni tuliamini ardhi tuliyoishi tungali wadogo huko Ngorongoro ilikuwa kila kitu kwetu, sasa tunaondolewa twende wapi?" aliuliza Laigwanan Karani na kuongeza kuwa baada ya kuona Serikali inayo mipango mizuri, waliamua kwa hiyari yao kuondoka, na kumwambia Naibu Katibu, afikishe salaam zetu kwa Mama yetu Samia Suluhu Hassan kwakutujali, maana sasa tunaweza kufanya ufugaji na Kilimo.


Laigwanan huyo alieleza zaidi Kwa kusema hata watoto wanasoma katika shule zenye majengo mazuri na huduma ya afya ipo.

Akizungumza wakati wa kuhitimisha ziara hiyo Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Wakili Amoni Mpanju aliwahakikishia wananchi hao kuwa pamoja na kuboresha hali ya miundombinu inayoendelea Serikali inapokwenda kwenye Mpango wa Bima ya Afya kwa wote wataona namna bora ya kuweza kuhakikisha wananchi wa Msomera wanachangia na wanaingia kwenye mpango huo.

“Hapa kuna kaya zaidi ya 1,692 zenye wakazi zaidi ya elfu 9, ni rai yetu kuona Uongozi wa Wilaya chini ya Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama Mhe. Mkuu Wilaya,Wakili, Dkt. Albert Musando, tunapokwenda kwenye Bima ya Afya kwa wote basi wananchi wa Msomera waweze kujiunga.

Wakili Mpanju aliongeza Kwa kusema kwani Muswaada wa Bima ya Afya Kwa wote sasa unakwenda kupitishwa na Bunge na kuwa sheria.


Katika hatua nyingine Wakili Mpanju, amewaambia wananchi hao kuwa katika kuhakikisha Wananchi wanajiletea maendeleo, watawatumia Maafisa Maendeleo ya Jamii waliopo kwenye eneo husika kwa shabaha yakuchechemua Maendeleo kwenye vikundi mbalimbali vya kiuchumi na wajasiriamali.

“Jiungeni kwenye vikundi ili muweze kujipatia Mikopo ya asilimia 10 kutoka Halmashauri ya Wilaya HANDENI lakini pia kupitia Wizara yetu, ipo Mikopo hadi ya mtu mmoja mmoja hizi zote ni fursa ambazo niwaombe Wana- Msomera mzichangamkie” alisema Wakili Mpanju.

Awali akimkaribisha Naibu Katibu Mkuu, Mkuu wa Wilaya ya Handeni, Wakili Dkt Albert Msando alisema anaishukuru Serikali kwa uboreshaji wa huduma mbalimbali za kijamii na yeye Kwa nafasi yake atasadiana na viongozi wenzake kuendeleq kuziimarisha huduma hizo ikiwepo mabweni kwa wanafunzi.


“Serikali imefanya kazi kubwa ya kuboreshea miundombinu, lakini yapo ambayo sisi kama Wilaya tumeona tutaendelea kuyaboresha zaidi ikiwepo ujenzi wa mabweni ili watoto wetu wapate muda mwingi wa kusoma , sambamba na hilo, kwakuwa huku ni jamii ya wafugaji, ni lazima sasa tuwabadili wanafunzi wetu kwa kuwajengea maboma ya Ng’ombe ili waweze kujifunza ufugaji wa kisasa” alisema Msando.

Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum kwa Ushirikiano na Wizara za kisekta pamoja na wadau wa Mandeleo zikiwepo Benki ya Azania na NMB, wamefanya ziara kwenye Kijiji cha Msomera, huku watoa huduma za Kibenki wakionesha dhamira ya kufikisha huduma zao Kijijini Msomera.

No comments:

Post a Comment