Na Kitengo cha Mawasiliano Mkoa wa Dodoma
Kikao hicho kimejadili ajenda mbalimbali zinazohusu masuala ya lishe kwa wanafunzi mashuleni ambayo ndio imekua ajenda kuu katika kikao cha mwaka huu.
Suala lishe kwa wanafunzi limepewa kipaumbele katika vikao vya Mkoa kwakuwa limebeba ustawi wa elimu kwa Mkoa kama anavyosisitiza Katibu Tawala Mkoa wa Dodoma Dkt. Fatuma Mganga
“Suala la lishe ni mtambuka na linahusisha kila sekta. Msisitizo uliopo sasa ni lishe mashuleni kuhakikisha wanafunzi wanapata chakula na hii itasaidia kupunguza utoro ambao ndio tunapambana nao kila wakati. Asilimia 27 ya watoto ndio wanapata chakula shuleni mpaka sasa. Tulishaweka azimio kila shule ilime kuhakikisha watoto wanapata chakula. Tuna wajibu wa kuwafundisha watoto kulima. Tunategemea kila shule itakua na hazina ya kutosha ya kutunzia chakula kwa mwaka mzima na hapo tutakua tumefanikiwa kudhibiti utoro mashuleni na kuinua kiwango cha taaluma” Amesema Dkt. Mganga
Hatahivyo, Mganga Mkuu wa Mkoa Dkt. Bestie Magoma ambaye pia ni mjumbe wa Kamati ya lishe Mkoa amesema kuwa suala la lishe linahitaji ushirikiano mkubwa kati ya Mkoa na Halmashauri zake ili maazimio yanayowekwa kwenye vikao hivi yaweze kutekelezeka na kuleta tija.
“Halmashauri moja ikifanya vibaya ni Mkoa mzima na hakuna Mkoa bila Halmashauri, nitoe rai, tuendelee kushirikiana na kwa pamoja kwani tunaona maendeleo yanayopigwa sasa kwenye kupunguza udumavu na lishe inaonekana inakwenda kuboreka hivyo tuendelee kushirikiana” Amesema Dkt. Magoma
Akihitimisha kwa kutoa maazimio yaliyofikiwa na wajumbe wa kikao hicho, Mkuu wa Wilaya ya Bahi Mhe. Godwin Gondwe, amesema.
“Kikao kiangalie viashiria vya lishe vilivyotolewa, elimu ya lishe iwe endelevu kwa kushirikisha viongozi wa ngazi zote, tusimamie mikakati ya watoto kupata chakula shuleni na kuimarisha miundombinu ya uvunaji maji ya mvua. Mhe. Mkuu wa Mkoa atatembelea maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya vituo vya lishe, asilimia 7.1 ya uwiano wa urefu na uzito kwa watoto upungue kufikia asilimia 3 na siku 1000 ni muhimu kwa lishe ya mtoto” Mhe. Gondwe
Baaadhi ya ajenda nyingine zilizojadiliwa kwenye kikao hicho ni pamoja na kukosekana kwa miundombinu rafiki kwa ajili ya unyonyeshaji watoto wachanga, uwasilishwaji wa maeneo kwa ajili ya kuchimba mabwawa ya kuhifadhi maji, kukosekana kwa miradi midogo midogo katika mipango ya Halmashauri, baadhi ya jamii kukosa elimu ya masuala ya lishe, baadhi ya kaya kukosa bustani za mbogamboga, baadhi ya Halmashauri kutoshirikisha viongozi wa dini katika masuala ya lishe na baadhi ya Halmashauri kutoingiza kwa wakati taarifa za utoaji wa matone ya vitamin ‘A’ kwa watoto wenye umri chini ya miaka mitano wakati wa kampeni.
No comments:
Post a Comment